Derby ya Simba Qeens na Yanga Princess kazi ipo!
Watani wa jadi Simba Qeens na Yanga Princess wanatarajia kushuka dimbani siku ya jumapili ya tarehe 24 Aprili, 2022 majira ya sa 10.00 za jioni katika dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam ikiwa ni mzunguko wa 15 wa ligi kuu ya wanawake ya Serengeti Lite.
Makocha wa timu zote mbili wametambiana huku kila mmoja akisema anamuheshimu mwenzake. Kocha Sebestian Mkomwa wa simba Qeens alisema wanaendelea na mpango wao waliojiwekea wa kucheza ligi na kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo, hivyo mpango wao bado uko palepale na anamshukuru Mungu mzunguko wa kwanza ulimalizika vizuri.
“Sasa tupo katika mzunguko wa pili na mkakati wetu ni kucheza michezo sita ya mwanzo vizuri ambayo itatufikisha katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa, kiujumla kuelekea katika ‘derby’ kimbinu tuko vizuri na kikosi kiko katika hali nzuri, tunasubiri siku ya mchezo ifike” alisema Mkomwa.
Kocha wa Yanga Princess Edna Lema alisema “Sisi kama timu tumejiandaa vizuri na hakuna maandalizi ya tofauti sana yaliyofanyika kwa sababu tu tunaenda kucheza na simba kwa maana ya kwamba timu zote mbili ziko kwenye ligi hivyo zote ni bora na ni timu kubwa , kiujumla kikosi changu kipo tayari kukabiliana na simba licha ya kutokuwa na matokeo mazuri katika michezo ya nyuma lakini naamini katika mchezo wa keshokutwa mambo yatakuwa tofauti” alisema kocha Edna.
Edna hakuacha kugusia changamoto ambazo kikosi kinapita kwa hivi sasa ikiwa ni pamoja na kuwakosa baadhi ya wachezaji wake ambao wamekwenda kujiunga na jeshi, Aisha Masaka ambae ameuzwa katika timu ya BK Hacken ya nchini Sweden pamoja na majeruhi wanne ambao watakuwa nje mpaka msimu utakapomalizika. Licha ya changamoto hizo haimaainishi kwamba hana timu ya kwenda kucheza na Simba na hatokubali kupoteza katika mchezo huo.
Fatuma Issa Maonyo maarufu kama Fetty densa ambae ni nahodha wa simba Qeens alisema hakuna mchezaji yoyote mwenye wasiwasi na mchezo wa jumapili kwa sababu ya maandalizi waliyofanya na wanaamini wanakwenda kuondoka na alama tatu
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Neema Charles wa Yanga Princess alisema kama wachezaji wamejiandaa vizuri na benchi la ufundi limeshamaliza kazi yake imebaki sehemu yao kwenda kufanya kile walichoelekezwa na waalimu wao.
Katika msimamo wa ligi kuu ya wanawake vinara ni Simba Qeens inayoongoza kwa alama 42 baada ya kucheza michezo 14 wakati Yanga Princess inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 32 katika michezo 14 ambayo tayari wamecheza.