Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.

Young Africans Yaibuka Mabingwa Wapya wa FA Arusha

Timu ya Young Africans imefanikiwa kutwaa Kikombe cha FA (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuifunga Coastal Union ya Tanga kwa penati 4-1 katika mchezo wa fainali ya kukata na shoka uliopigwa Julai 2, 2023 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha.

Mchezo huo uliopigwa mnamo majira ya saa tisa alasiri ulifikia hatua ya mikwaju ya penati baada ya timu hizo kutoshana nguvu ndani ya muda wa kawaida, na hata baada ya kuongezwa kwa dakika 30 bado matokeo yalikuwa sare ya 3-3.

Mabao yote ya Coastal Union yalifungwa na Abdul Sopu (JN.9); goli la kwanza lilifungwa dakika ya 11 ya mchezo huo; goli hilo likisawazishwa na Feisal Salum kwenye dakika ya 58 ya kipindi cha pili kabla ya Heritier Makambo kupachika bao la pili kwa Young Africans kunako dakika ya 83; bao hilo lilisawazishwa na Sopu mnamo dakika ya 89 na kuzifanya dakika 90 kutamatika kwa matokeo ya 2-2.

Dakika 30 za kumsaka bingwa mpya zilikuwa za moto kwa kila timu; kwani kulikuwa na mashambulizi makali kutoka kila upande; mnamo dakika ya 99 mchezaji Abdul Sopu aliwainua kwa mara ya tatu mashabiki wa Coastal Union baada kushindilia bao la 3 lililowanyong’onyeza mashabiki wa Young Africans kabla ya Denis Nkane kuandika bao la kusawazisha kwenye dakika ya 113 bao lililozifanya dakika 120 ziendelee kushindwa kuamua mchezo huo baadala yake kwenda kuamuriwa na matuta 4-1.

Akizungumza baada ya fanali hizo kocha msaidizi wa Young Africans Cedric Kaze alisema wao kama benchi la ufundi na linaloongozwa na Mohammed Nabi, pamoja na wachezaji wote wamefurahi kufikia malengo waliojiwekea ya kutwaa vikombe vyote vitatu Ngao ya Jamii, Ligi Kuu ya NBC na Kikombe hicho cha Azam (ASFC).

Kocha Kaze aliongeza kwa kuwapongeza wachezaji wote kwa namna walivyojituma ili kuitafutia ushindi muhimu timu yao. Alisema kuwa haikuwa kazi ndogo kwani mashindano hayo yalikuwa na ushindani mkubwa hasa kwa msimu huu 2021/2022 ambapo kila timu waliyokutana nayo ilikuwa imejipanga sawa sawa kupata matokeo, jambo ambalo liliwapa ugumu licha ya kufanikiwa kutwaa ubingwa huo.

Kwa upande wake kocha wa Coastal Union Juma Mgunda, yeye alikiri kuwa mchezo huo wa fainali ulikuwa mgumu kwa timu zote na kwamba wachezaji wake walipambana lakini bahati haikuwa kwao kwani walifanikiwa kuongoza, bahati mbaya wakafanya makosa yaliyowapatia nafasi ya kurejesha mabao yote wapinzani wao na hivyo kuwarejesha mchezoni; jambo lililowafanya wafike kwenye mikwaju ya penati ambayo Young Africans walitumia uzoefu na kuibuka mabingwa.

Mbali na hayo, Mgunda alimpongeza mchezaji wake kinda Abdul Suleiman Sopu kwa kufunga mabao matatu dhidi ya timu kubwa na kwenye mchezo muhimu wa fainali. Hata hivyo, kocha Mgunda alisema msimu umekwisha, kinachofuata ni wao kwenda kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao wa 2022/2023.

Kwa upande wake mfungaji na mchezaji bora wa mchezo huo wa fainali Abdul Sopu alieleza furaha yake ya kufanikiwa kupachika mabao 3 peke yake, huku akidai kuwa bahati haikuwa kwao ndiyo maana walishindwa kutwaa ubingwa huo ambao ulikuwa na umuhimu mkubwa kwao. Naye nahodha wa Young Africans Bakari Mwamnyeto alishukuru kwa kubeba ubingwa huo na pia kupeleka salamu kwa mashabiki kuwa wameisha lipa deni na kwamba hawadaiwi chochote isipokuwa kilichobaki ni kwenda kujipanga zaidi ili waweze kufanya vyema kwenye msimu ujao wa 2022/2023.

Young Africans ilifanikiwa kufika hapo baada ya kuitoa Simba SC kwa bao 1-0 huku Coastal Union nao wakiwafuata kwenye fainali baada ya kuifurusha Azam FC kwa mikwaju ya penati(5-6) ikiwa ni baada ya dakika 90 kushindwa kuamua nani anakwenda fainali. Kukumilika kwa mashindano hayo ya FA ndiyo kunaashiria kutamatika rasmi kwa msimu wa 2021/2022 na hivyo timu zote sasa zitageukia kwenye usajili kwa ajili ya kujiandaa kwa msimu mpya wa 2022/2023.

 

Did you find apk for android? You can find new Free Android Games and apps.