TFF yaendesha semina ya usajili na uhamisho wa Kimataifa.
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (Tff) limeendesha semina maalum Kwa ajili ya kukumbushia taratibu za Usajili na uhamisho wa Kimataifa (FIFA CONNECT & TMS) Leo Julai 11,2022 katika moja ya kumbi za mikutano zilizopo katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Semina hiyo yenye lengo la kutatua changamoto za usajili na kuvihimiza vilabu kukamilisha usajili wa wachezaji kwa wakati katika kipindi hiki cha dirisha kubwa la usajili lililofunguliwa rasmi julai 1, 2022 na litafungwa tarehe 30, Agosti 2022.
Akizungumza katika semina hiyo meneja mashindano wa TFF Baraka Kizuguto aliwataka mameneja usajili wa vilabu vyote kuzingatia taratibu zilizowekwa na kuhakikisha wanatimiza vigezo vyote vya usajili ikiwa ni pamoja na kuambatanisha nyaraka tano muhimu zinazohitajika wakati wa usajili ambazo ni cheti cha kuzaliwa endapo mchezaji yuko chini ya miaka 18, juu ya miaka 18 lazima awe na kitambulisho cha uraia, mkataba wa stahiki za mchezaji, vipimo vya utimamu wa mwili na afya ya mchezaji kwa ujumla na huku akisisitiza vipimo vifanyike kwa usahihi pamoja na picha ya pasipoti ya mchezaji.
Kuhusu uhamisho wa wachezaji meneja huyu alisema” ni vyema kufanya mawasiliano na klabu husika ya mchezaji kulingana na kanuni zinavyosema (kanuni ya 70 ya usajili) ili kupunguza kesi za mikataba ambazo kwa upande wa ligi kuu kesi hizo zimepungua kwa kiasi kikubwa, hivyo umakini katika usajili uongezeke na hakutakuwa na muda wa ziada baada ya dirisha kufungwa”.
Semina hiyo imewahusisha mameneja usajili wa vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya NBC, championship, First League na ligi kuu ya wanawake ya Serengeti Lite.