kozi ya Caf A Diploma yaendelea kwa Mkapa
Moduli ya tatu ya kozi ya CAF A diploma imeanza leo katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam baada ya moduli ya pili kumalizika mwezi Mei, 2022 na washiriki kuelekea katika mafunzo kwa vitendo katika timu za taifa na vilabu wanavyotumikia.
Kozi hiyo ya siku 10 inajumuisha washiriki 25 kutoka nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Zambia na kenya, huku Tanzania ambaye ni mwenyeji wa kozi hiyo baada ya kukidhi vigezo vya CAF vya kuendesha kozi za juu za ualimu wa Mpira wa miguu ikitoa washiriki 19.
Mkufunzi wa kozi hiyo Ulrich Mathiot alisema “kiujumla moduli ya tatu ya Kozi hii itajikita zaidi katika kusikiliza na kupitia mrejesho wa kile walichokifanya wakati wa mafunzo kwa vitendo ili kubaini changamoto walizokutana nazo na kuzijadili kwa pamoja ili kuzipatia suluhisho. Vilevile kushirikishana uzoefu hasa ukizingatia washiriki wanatoka katika nchi tofauti tofauti.
Kozi hii ilianza kutolewa Agosti 2,2021 katika makao makuu ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania ikiwa ni mara ya kwanza kwa kozi ya taaluma ya juu katika ualimu wa mpira kufanyika nchini Tanzania huku ikitarajiwa kumalizika mwezi Agosti mwaka huu.