Ruvu Shooting, Prisons Hakuna Mbabe Uhuru
Mchezo uliozikutanisha timu za Majeshi Ruvu Shooting dhidi ya Tanzania Prisons umemalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliopigwa Novemba 7, 2022 mnamo majira ya saa 10:00 jioni, Ruvu Shooting ndiyo walikuwa wenyeji wakiwalika Prisons kutoka Mbeya ambao waliwapa usumbufu mkubwa wa kuondoka na matokeo chanya kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Magoli yote ya timu hizo yalipatikana katika kipindi cha pili; goli la Prisons lilipachikwa na Samsoni Mbangula mnamo dakika ya 48 huku Ruvu Shooting wakisawazisha bao hilo kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Adulkassim Suleiman katika dakika ya 56 ya kipindi hicho cha lala salama.
Baada ya mchezo huo kocha Boniface Mkwasa wa Ruvu Shooting alisema timu yake imecheza vizuri licha ya kushindwa kutumia vyema nafasi nyingi walizozitengeneza ambazo endapo wangeongeza umakaini basi wangeweza kuibuka na alama zote tatu.
Hata hivyo, Mkwasa alisema mechi bado nyingi hivyo watakuwa wakiimarika siku hadi siku na kwamba anauhakika katika michezo ijayo kikosi chake kitafanya vizuri zaidi ili kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Wakati Mkwasa akisema hayo, kwa upande wake Patrick Odhiambo kocha wa Tanzania Prisons yeye alisema wameyapokea matokeo na kwamba watakwenda kuyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo ili waweze kuendelea kupata matokeo chanya katika michezo mingine.
Aliongeza kuwa Ligi Kuu ya NBC imezidi kuwa ngumu pengine kuliko msimu uliopita kwani kila timu imejipanga zaidi kupata matokeo jambo ambalo limeongeza ushindani na hivyo kuhitaji mbinu za ziada katika kuyapata matokeo chanya.
Kwa matokeo hayo Ruvu Shooting anabakia katika nafasi yake 12 akifikisha alama 11 kwenye michezo 11huku Tanzania Prisons wao pia wakisalia katika nafasi ya 8, baada ya kuvuna alama 1 kwenye mchezo huo wa ugenini na kufikisha alama 14 wakiwa wameshuka dimbani mara 10 mpaka sasa.