Young Africans Yawaduwaza Waarabu Yatinga Makundi Shirikisho
Timu ya Young Africans imefanikiwa kutinga hatua ya Makundi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Club Africain ya Tunisia katika mchezo wa marudiano uliopigwa nchini Tunisia Novemba 09, 2022.
Bao la dakika ya 79 lililofungwa na Kiungo Mshambuliaji wa Kimataifa Stephane Azizi Ki (10) akitokea benchi lilitosha kuiengua Club Africain na kuipeleka Young Africans kwenye hatua ya makundi katika michuano hiyo ya daraja la pili kwa ukubwa ukiachana na ile ya Klabu Bingwa Afrika ambayo kwa Tanzania timu ya Simba ndiyo imefanikiwa kuingia kwenye hatua kama hiyo ya 16 Bora.
Mchezo huo ulipigwa Tunisia majira ya saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kati ya timu hizo ulikuwa ni wa duru ya pili ambapo katika mchezo wa awali kocha Nabi alisema kuwa ulikuwa mchezo wa pili ulikuwa bado ni hamsini kwa hamsini kutokana na mchezo wa kwanza uliopigwa kwa Mkapa jijini Dar es Salaam kumalizika kwa suluhu tasa. Hata hivyo, Young Africans walikuwa na nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele kufuatia wao kutoruhusu bao lolote kwenye uwanja wa nyumbani jambo lililowapatia machaguo mengi zaidi ya wapinzani wao.
Young Africans walihitaji ushidi wowote ama sare ya kufungana ili waweze pita, wakati wenyeji Club Africain wao walihitaji ushindi pekee, kwani matokeo ya suluhu tasa yangelipeleka mchezo huo kwenye changamoto ya mikwaju ya penati ambayo kimsingi hatua hiyo huwa haina mwenyewe.
Baada ya mchezo kumalizika kocha wa Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi alisema kuwa kikosi chake kilijitahidi kufuata maelekezo vema hasa baada ya kwenda kwenye mapumziko huku milango yote ikiwa migumu. Lakini mara baada ya kurejea kwenye ngwe ya pili mahesabu yakaenda sawa na ndiyo maana wakaweza kuibuka washindi wa mchezo huo.
Timu ya Young Africans itakuwa timu ya pili kufuzu michuano ya CAF na timu pekee inayopeperusha Bendera kwenye Kombe la Shirikisho ikiifuata Simba ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikifanya vizuri zaidi katika michuano ya CAF.
Aidha, katika hatua nyingine, Simba Queens ilikuwa ikimenyana vikali na Mabingwa watetezi wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika kwa timu za Klabu ambapo licha ya kutokutinga katika hatua ya fainali bado Simba ilionesha kandanda safi kilichowafanya Mabingwa watetezi Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 kwa taabu.
Simba Queens watashuka tena uwanjani siku ya Juma Mosi ya Novemba 12, 2022 kwa ajili ya kuisaka nafasi ya tatu katika michuano hiyo baada ya kupoteza mchezo wa nusu fainali ambapo atakutana na timu yeyote kati ya AS FAR ya Morocco ambao ndiyo wenyeji, au timu ya Bayelsa Queens ya nchini Nigeria.
Kitendo cha Simba Queens kutinga tubhatua ya Nusu Fainali katika Klabu Bingwa Afrika ni ishara tosha kuwa sasa Tanzania imepiga hatua kubwa katika soka la wanawake kuanzia kwenye klabu mpaka timu za Taifa..kwani uwepo wa timu bora au wachezaji bora ndiko kunachangia kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa vikosi bora vya timu za Taifa.