Simba Young Africans Bado Zina Nafasi CAF
Michezo kadhaa ya Mashindano ya CAF ilipingwa wikiendi hii huku wawakilishi pekee wa michuano hiyo Simba na Young Africans wakifanikiwa kupata matokeo chanya ambayo yanatoa matumaini ya kusonga mbele endapo watafanikiwa kupata alama katika michezo miwili kati ya mitatu iliyosalia.
Timu ya Simba ilifanikiwa kupata alama 3 baada ya kuiadhibu Vipers FC kwa bao 1-0; bao hilo likipachikwa nyavuni na beki wa kikosi hicho Heneck Inonga Baka (Veran) aliyefunga bao hilo mnamo dakika ya 20 kipindi cha kwanza nakuifanya timu hiyo kupata matumaini ya kuweza kusonga mbele.
Mchezo huo kati ya Simba na wenyeji Vipers FC uliopigwa Februari 25, 2023 ambapo timu ya Simba iliingia uwanjani ikihitaji matokeo ya ushindi pekee ili kufufua matumaini yao baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye michezo miwili ya awali; nyumbani dhidi ya Raja Casablanca na ule wa ugenini uliowakutanisha na Horoya FC ya Genea.
Kocha Wa Simba Robertnho Oliviera alisema ushindi walioupata umechagizwa na utayari wa kila mchezaji wa kuipambania timu yao, huku akitanabaisha kuwa mbinu mpya ya 4-4-2 aliyoitumia katika michezo huo ambapo kocha huyo Mbrazili aliwatumia akina Saido, Moses Phil na Kibu Denis ndiyo iliyowachanganya Vipers; kwani walijikuta wanashindwa kujua mshambuliaji halisi ni nani ndani ya watatu hao waliolisakama lango kwa pamoja.
Kwa upande wa Young Africans wao walishuka dimbani kuminyana na wenyeji Real Bamako FC, nchini Mali ambako waliwalazimisha wenyeji hao sare ya bao 1-1. Katika mchezo huo Young Africans ndiyo waliotangulia kuandika bao; bao hilo likifungwa na mshambuliaji raia Wa Kongo, Fistone Kalala Mayele kunako dakika ya 60 kipindi cha pili. Baadaye wenyeji hao waliamka na kuandika bao la kusawazisha mnamo dakika 89 kipindi hicho cha pili kupitia Emile Kone; bao hilo likizifanya timu hizo kugawana alama 1-1.
Matokeo hayo yanafaida kwao kuwa wameyapatia ugenini, hivyo wanatarajia kupambania alama sita katika michezo yao miwili ya nyumbani ambapo mchezo wa moja unatarijiwa kuchezwa Machi 8, 2023 na mwingine dhidi ya Monastir kabla ya kwenda kumalizana na TPMazembe Lubumbashi Kongo katika mchezo wao wa sita.
Timu hizo za Simba na Young Africans zinatarajiwa kushuka dimbani Machi 7 na 8, 2023 tayari kutupa karata zao huku wanachama, wapenzi na wadau wa timu hizo wakitarijia kupata ushindi.