Rais Samia aahidi kutoa tiketi 2000 kwa mashabiki wa Taifa Stars
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kutoa tiketi 2000 kwa mashabiki wa Taifa Stars kwa ajili ya kwenda kushuhudia mchezo wa marudiano wa kufuzu AFCON Kati ya Taifa Stars dhidi ya Uganda utakaopigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 28,2023.
Mheshimiwa Rais Ametoa ahadi hiyo kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika mkutano na wanahabari ulioandaliwa na TFF uliobeba jina la ‘Jambo la nchi’ uliofanyika katika hoteli ya Tiffany Diamond jijini Dar es Salaam.
Akiongea kwa njia ya simu Mheshimiwa Waziri mkuu alisema “ni fursa kubwa ambayo tutaipata endapo timu yetu itafuzu kushiriki AFCON kwasababu hadhi ya taifa letu itapanda lakini pia tutapanda katika viwango vya soka Duniani. Kwa kutambua umuhimu huo Rais ameniagiza niseme kuwa atatoa tiketi 2000 kwa ajili ya mashabiki kwenda kutazama mechi ya marudiano itakayochezwa hapa nyumbani”.
Mbali na kuwasilisha ujumbe wa Rais Samia, Waziri Mkuu aliongeza tiketi 2000 kwa ajili ya mashabiki na kufanya jumla ya tiketi zilizotolewa na serikali kufikia tiketi 4000.
Wadau wengine wa soka walijitokeza kutoa ahadi za kununua tiketi kwaajili ya mashabiki ambao ni mwenyekiti wa DRFA Lameck Nyambaya (200), Rais wa klabu ya Young Africans Engineer Hersi Said (1500) Afisa mtendaji mkuu wa Azam Abdulkarim Amin (1000),Mwenyekiti wa klabu ya Simba SC Murtaza Mangungu (600), Naibu Waziri wa kilimo Mheshimiwa Antony Mavunde (200), Mkuu wa mkoa wa Njombe Mheshimiwa Antony Mtaka (200).
Wengine ni Mbunge mstaafu wa Jimbo la Kinondoni Idd Azzan (300), Abdallah Mwaipaya Mkuu wa wilaya ya Mwanga (100), Mmiliki wa Kitambaa cheupe Jessica kikumbi (300), Hashim Mbaga Mwakilishi wa Swahili water (100), Lampard electronics (100), Bullet Force (100) na wengine wengi.
Jumla ya tiketi 10,500 zilipatikana katika mkutano huo, huku Ofisa habari wa TFF Clifford Ndimbo pamoja na wasemaji wa klabu mbalimbali ikiwemo Simba SC, Young Africans pamoja na Azam FC wakihimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu ya taifa ya Tanzania ili iweze kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa.