Tanzania, Nigeria zatoshana nguvu Azam Complex, Chamazi
Timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 ‘Tanzanite Queens’ Leo Novemba 12, 2023 imetoka sare ya goli 1-1 dhidi ya timu ya Nigeria katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia uliochezwa katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi majira ya saa 9 Alasiri.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu zote mbili kutokuona lango la mwenzake licha ya timu ya Nigeria kuonekana kumiliki mpira kwa muda mrefu. Ni timu ya Nigeria ndio ilikuwa ya kwanza kupata goli la kuongoza kupitia kwa mchezaji Chioma Olise ( DK 57) na baadae Tanzania ikapata goli la kusawazisha DK 71. Goli la Tanzania lilifungwa na mchezaji Hasnath Ubamba.
Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika Kocha mkuu wa ‘Tanzanite’ Queens’ Bakari Shime alisema hatujapata matokeo mazuri licha ya kwamba timu ilicheza vizuri na ilikuwa katika uwanja wa nyumbani lakini bado tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano.
” Tuliingia tukiwaheshimu Nigeria ili wasije kutuadhibu kwa magoli mengi lakini sasa tumeona aina yao ya uchezaji tunakwenda kujipanga kwa siku zilizobaki na kurekebisha makosa tuliyoyafanya ili tuweze kupata ushindi ugenini na kusonga mbele katika raundi ya nne” alisema Kocha Shime
Naye kocha wa Nigeria Christopher Musa Danjuma aliema mpira wa miguu kwa wanawake umebadilika sana kila nchi inazidi kuwa bora hivyo Tanzania ni timu bora ambayo imeonyesha ushindani mkubwa ambao hakuwa ameutegemea hapo awali.
Mchezo wa marudiano kati ya Nigeria dhidi ya Tanzania utachezwa Novemba 19, 2023 nchini Nigeria.