Mkutano Mkuu wa 10 wa bodi ya Ligi Kuu Tanzania umefanyika Disemba 8, 2023 kwenye ukumbi wa mikutano wa bodi hiyo na Mgeni Rasmi akiwa ni Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo nchini Mh. Damas Ndumbaro.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa soka akiwepo Katibu Mkuu Mtendaji wa (BMT) Neema Msitha na Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred.
Akifungua mkutano huo wa 10 mgeni rasmi, Mh Ndumbaro aliisisitiza bodi ya ligi na TFF kuendelea kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha ligi kuu inakuwa namba moja Afrika.
Alisema Katika miaka 10 bodi ya ligi imefanya mambo mengi mazuri, ikiwa ni pamoja na kutoa ligi katika nafasi ya 10 hadi hadi kuwa ligi ya 5 kwa ubora Afrika huku akiwataka kuweka mkakati wakuifanya iwe namba moja.
Aidha alisema ubora wa ligi kuu ndio umefanya hivi karibuni CAF ikatuamini na kutupatia uwenyeji kwenye ufunguzi wa mashindano mapya ya African Football Leagu na kuwataka watanzania na wadau wa soka kuwasifu, kujivunia pamoja na kuunga mkono utendaji na usimamizi bora kwenye sekta hiyo ya mpira wa miguu.
Kwa upande wa ligi Kuu Tanzania Afisa Mtendaji Mkuu Almasi Kasongo alisema kupitia mkutano huo wanaamini watakwenda kufikia maazimio yao kwa mwaka ujao kama ambavyo taratibu zao zilivyo za kuboresha kila mwaka.
Alizitaka timu zote kuzingatia utekelezaji wa club licencing huku akisisitiza timu hizo kusimamia maeneo matano yanayounda club licence hasa katika kuimarisha uchumi wa klabu na kudhibiti madeni ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma hadhi ya klabu na ligi kwa levo ya Kitaifa na kimataifa.
Hata hivyo mkutano huo mkuu wa 10 wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ulihudhuliwa na viongozi mbalimbali kutoka TFF na Bodi ya ligi pamoja na viongozi waliowakilisha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC, Ligi ya Championship na First Division League.