Pawasa: “Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni Nafasi Bado Ipo”
Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni Boniface Pawasa na wachezaji wa timu ya hiyo kwa pamoja wamesema kuwa Tanzania bado inanafasi ya kusonga mbele katika michuano COSAFA inayoendelea nchini Afrika Kusini kuelekea mchezo wa mwisho dhidi ya Morocco.
Akizungumza baada ya mazoezi ya mwisho yaliyofanyika uwanja wa South Beach Arena Kocha Pawasa alisema tofauti ya alama na wapinzani wao kwenye kundi haiwatishi, bado anaimani kubwa na kikosi chake na kwamba wanahitaji kupambana kwenye mchezo huo wa mwisho.
“Morocco wanaongoza kundi, ila sisi tukifanikiwa kuifunga kwa magoli mengi tutakuwa na faida ya kusonga mbele lakini pia matamanio yetu ni kuweka heshima kwa kuifunga timu kubwa inayoongoza Afrika” alisema kocha.
Kwa upande wa wachezaji nahodha wa timu hiyo Jaruph Juma alisema kwa upande wao morali bado ipo juu na imani ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo ipo juu zaidi.
“Mchezo dhidi ya Morocco utakuwa ni mzuri na mgumu kutokana na timu tunayokwenda kukutana nayo kuwa tunaifahamu. Morocco ni timu bora kama ambavyo sisi tulivyo bora hivyo tumejiandaa vizuri morali ipo juu kwetu wachezaji lakini pamoja na benchi la ufundi sote tunamtazamo chanya kuwaendea wapinzani wetu” alisema Jaruph.
Timu hiyo ya Taifa Soka la Ufukweni itashuka dimbani South Beach Arena Machi 20, 2024 majira ya saa 11:00 jioni kutafuta nafasi ya kusonga mbele kwenye mashindano hayo ya COSAFA dhidi ya Morocco.