Jasho Lamwagika Msimu Mwingine wa Vijana
Msimu mwingine Kwa vijana umeanza Kwa Kasi huku TFF ikiendesha Ligi mbili za (U17 Premier league na U17 Championship league 2023-2024), zikiwa ni ligi mbili zinazohusisha takribani timu 28 za vijana kutoka Tanzania bara.
Timu 14 za vijana zikiwemo zile zinazowakilisha timu kubwa zinazoshiriki Ligi kuu ya NBC zinashiriki Ligi kuu ya vijana U17, na timu nyingine 14 zinashiriki Championship Kwa vijana zikiwemo timu zinazowakilisha timu kubwa zinazo cheza Ligi ya NBC Championship.
Ligi zote hizo zilizoanza kutimua vumbi Aprili 19, 2024 zimekamilisha raundi ya pili Kwa michezo iliyotimua vumbi mwishoni mwa wiki hii kwenye viwanja vya TRA Mivinjeni na Kituo cha Ufundi Cha TFF Kigamboni jijini Dar es salaam.
Mpaka sasa msimamo wa Ligi kuu unaongozwa na timu tatu zilizofungamana alama, Simba SC ikiwa Kileleni Kwa tofauti ya goli 1 na Azam FC iliyo nafasi ya pili Kwa faida ya magoli 5 ikifuatiwa na JKT Tanzania ambayo pia ina alama 6. Huku timu tatu (Tanzania Prison, Tabora United na Mtibwa Sugar FC) zikiburuza mkia baada ya kupoteza kwenye mechi zote mbili.
Wakati vita ya ligi kuu ikiwa Bado katika kutegeana na kusemana baina ya timu hizo, huko Championship timu ya TDSU15 yenyewe imeanza kutembeza kichapo mapemaa baada ya kushinda Kwa kishindo kwenye mechi yake ya mzunguko wa pili dhidi ya Pan African na kusimamia Kileleni mwa msimamo wa Ligi Kwa kufikisha jumla ya alama 6 sawa na Copco FC iliyonyuma Kwa tofauti ya magoli 5.
Hata hivyo ndio kwanza vijana wameanza kumwagika jasho kupigania timu zao ambapo Ligi hizo zote zinatarajia kuendelea kutimua vumbi Kwa mzunguko wa tatu kuanzia Mei 3, 2024 kwenye viwanja vilivyoko kituo cha ufundi cha TFF Kigamboni.