Amos Makala: Rais Karia Ameandika Historia Mpya

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makala amesema Rais wa TFF Wallace Karia ameandika historia mpya kwa kutekeleza kikamilifu na kwa vitendo vipaumbele vyote alivyoviainisha wakati anaingia madarakani mwaka 2017.

Ameyasema hayo leo Novemba19, 2021 alipotembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha ufundi uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam; mradi huo unatekelezwa na TFF wakishirikiana na shirikisho la soka ulimwenguni (FIFA) ikiwa ni sehemu ya maboresho ya miundombinu kwa ajili ya ustawi wa soka la Tanzania.  Mradi wa Kigamboni unaenda sambamba na mradi ulioko Mnyanjani, jijini Tanga ambayo yote inalenga kuleta mapinduzi katika mchezo wa soka nchini.

Akizungumza  wakati akiwa eneo la mradi huo wa Kigamboni,  Mhe. Makalla alisema; ” nimefurahishwa na kasi ya ujenzi inavyokwenda na kila siku nimekuwa nikisikia kuhusu miradi ya FIFA lakini vitendo havionekani ila leo nimejiona kwa macho, hivyo nitoe pongezi Kwa Rais wa TFF na watendaji wake Kwa kuweza kufanikisha jambo kubwa ambalo halijapata kutokea hapa nchini.”

Mhe. Makalla aliongeza kwa kusema mradi huo utaokoa fedha nyingi ambazo hapo awali zilikuwa zikitumika kuwezesha shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukodi sehemu za malazi kwa wachezaji, viwanja vya kufanyika mazoezi, kukodi kumbi za kutolea mafunzo mbalimbali na nyinginezo. Hii ni kutokana kurahisha upatikanaji wa miundombinu hiyo yote katika eneo moja na linalomilikiwa na TFF wenyewe, lakini pia kwa upande mwingine itakuwa ni chanzo kipya cha mapato kwa watu wa nje watakaohitaji kutumia miundombinu hiyo kwa nyakati tofauti.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam, alihitimisha kwa kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa TFF muda na wakati wowote watakapokuwa na uhitaji; kwani yeye ni mdau mkubwa wa soka na anatamani kuona maendeleo ya soka la Tanzania, ikumbukwe kuwa Amos Makalla aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo katika Serikali ya Awamu ya Nne iliyokuwa chini ya uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Naye Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred alimshukuru Mhe. Amos Makalla kwa kuweza kufika katika eneo la mradi na kumhakikishia kwamba mradi utakamilika kwa wakati na kwamba taratibu zote za msingi kuhusiana na ujenzi wa mradi huo zinazingatiwa.

Hata hivyo, Katibu Mkuu hakusita kutoa ombi kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu ujenzi wa kipande cha barabara kinachoingia hadi katika eneo la mradi ili barabara hiyo iweze kupitika kiurahisi na kufanya mandhari ya eneo hilo iwe nadhifu. Ombi hilo kutoka kwa Kidao Wilfred lilikubaliwa na Mkuu wa Mkoa na kumuagiza kiongozi wa TARURA aliyekuwa ameambatana naye kushughulikia jambo hilo haraka iwezekanavyo.

Hatua ya kwanza ya Mradi wa Kigamboni ilianza kutekelezwa Oktoba 24, 2020 na mpaka hivi Leo mradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 70 ikijumuisha jengo la utawala, mabweni yenye uwezo wa kulaza wachezaji 208   kwa wakati mmoja, chumba cha kutolea  mafunzo (training) pamoja na viwanja viwili  vya mpira ambapo kimoja kitakuwa na nyasi bandia na kingine kitakuwa na nyasi za asili.