Azam FC Mabingwa Ligi ya TFF U17 2023

Azam FC imefanikiwa kubeba ubingwa ligi ya TFF Vijana chini ya miaka 17 kwa vilabu msimu wa 2022/2023.

Hatua ya Azam FC kutangaza ubingwa huo ni baada ya ushindi wa bao 4-0 dhidi ya timu ya African Sports kwenye mchezo wa raundi ya 14, matokeo yaliyoifanya Azam kufikisha alama 38 ambazo hazikuweza kufikiwa na washindani wake.

Hata hivyo licha ya Azam kujihakikishia ubingwa ilishinda tena 1-0 kwenye mchezo wa mwisho uliopigwa Agosti 3, 2023 Azam Complex dhidi ya Green Warriors, mchezo ambao Azam ilikabidhiwa kombe, huku ikiwa na rekodi ya kuwa ndio timu pekee ambayo haikupoteza mchezo wowote msimu huu.

Katika mchezo huo bao pekee la Azam FC lilifungwa na Mohammed Shilla katika Kipindi cha pili, bao lililo salia mpaka dakika 90 zinamalizika na kufanya Azam ipate ushindi wa bao 1-0.

Mbali na ubingwa huo pia Azam FC ilifanikiwa pia kubeba tuzo mbalimbali kwenye sherehe za ubingwa, ukiachana na tuzo ya kocha bora aliyobeba Mohammed Badru timu hiyo pia ilibeba tuzo ya mchezaji bora kupitia mchezaji Mohammed Shilla na tuzo ya golikipa bora aliyotunukiwa Abdurahman Vuai.

Azam FC pia ndio timu pekee iliyotunukiwa vyeti maalum na TFF ikiwa ni sehemu ya pongezi kwa kutwaa ubingwa huo, vyeti mbavyo nahodha alikabidhiwa na mgeni rasmi Makamu wa Rais TFF Athuman Nyamlani wakati wa sherehe hizo za ubingwa.