Azam FC Yapata Ushindi Jioni Nyumbani huku Simba Ikitakata Ugenini

Timu ya Azam FC imefanikiwa kupata ushindi wa bao 3-2 dhidi ya Coastal Union katika mchezo uliopigwa Novemba 27, 2022 majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wake wa Azam Complex Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa na ulianza kwa kasi huku Coastal Union wakifunguka na kufanya mashambulizi makali yaliyopelekea kupata bao la mapema lililofungwa na Maabadi Maulidi dakika ya 13 za kwanza, kabla ya James  Akaminko kuwasazishia bao hilo dakika ya 55 kwa kuachia  shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Coastal Union na kutinga nyavuni.

Dakika ya 71 ya mchezo, Yahya Zayd aliipatia Azam FC bao la pili akiachia shuti kali kabla ya Hammad Majimengi kuwasazishia Coastal Union bao hilo kunako dakika ya 84. Hata hivyo  wakati Coastal Union wakiwa na matumaini makubwa ya kutoka walau na alama moja, Iddi Sulemani Nado alirejesha furaha ya Azam FC dakika za jioni ama za lala kwa buriani (90+) na kuwafanya wana rambaramba hao kuibuka na ushindi wa jumala ya mabao 3-2.

Mchezo huo uliirejesha timu ya Azam FC katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikifikisha alama 32 sawa na vinara Young Africans wanaongoza kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.

Aidha, Mchezo mwingine wa mapema zaidi ulikuwa kati ya Simba SC na Polisi Tanzania, mchezo huo ulimalizika kwa timu ya Simba kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 ikiwa kwenye uwanja wa ugenini, Ushirika Moshi.

Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na John Bocco dakika ya 32 kipindi cha kwwnza, huku  Moses Phiri naye akiifungia timu yake hiyo  magoli mawili kati ya dakika ya 43, na 53 na kukamilisha karamu ya mabao kwa Wanamsimbazi hao. Bao pekee la kufutia machozi kwa upande wa timu ya Polisi Tanzania lilifungwa na Zuberi Mbogo mnamo dakika za lala salama (90+) likiufanya mchezo huo uliotawaliwa na Simba kwa kiwango kikubwa katamatika kwa matokeo ya mabao 3-1.

Matokeo hayo yanairejesha Simba SC katika nafasi ya tatu baada ya kuvuna alama 31 ikishuka dimbani mara 14 nyuma ya Azam FC yenye alama 32 nayo ikicheza michezo 14 sawa na Simba SC; zote zikiwa mbele ya Young Africans kwa michezo miwili.