Azam, Simba Zatakata Ligi Kuu Bara
Ligi Kuu ya NBC Bara imeendelea kwa michezo miwili kupigwa katika viwanja viwili tofauti; mchezo wa saa 10:00 jioni uliwakutanisha Mtibwa Sugar dhidi ya Azam FC huku ule wa pili ukiwa kati ya Ihefu FC na Simba SC majira ya saa 1:00 usiku kwa Mkapa.
Mchezo wa Manungu Morogoro, ulikuwa na mvua ya magoli; Azam FC walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4 huku Mtibwa wakifunga mabao 3. Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, kutokana na kila timu kufunguka. Azam ndiyo ilikuwa ya kwanza kuandika bao kupitia Idris Mbombo dakika ya 18 aliyerejea kambani kunako dakika ya 29 huku bao la 3 likifungwa na Abdallah Kheri dakika ya 40.
Mtibwa Sukari warerejea kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kuandika mabao mawili kupitia kwa Adam Adam aliyepachika mabao hayo dakika ya 61 na ya 75 huku bao la 3 likifungwa na Nassor Kiziwa mnamo dakika ya 77 ya mchezo baada ya Azam FC kuwa wameongeza bao la 4 na la mwisho kupitia kwa mlinzi wa kati Daniel Amoah kunako dakika ya 63.
Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha Salum Mayanga wa Mtibwa Sugar alisema wachezaji wake walijichanganya katika kipindi cha awali hasa kwenye safu ya ulinzi na kupelekea kuaadhbiwa mabao 3 ya mapema, lakini kipindi cha pili waliingia na mbinu mpya iliyowasaidia kupata mabao matatu. Mayanga aliahidi kuwa makosa yaliyojitokeza watayafanyia kazi ili waweze kushinda michezo inayofuata.
Kally Ongalla wa Azam FC aliwashukuru wachezaji kwa kujituma na kuweza kulinda ushindi maana mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa. Hata hivyo, kuna udhaifu alioubaini kwenye kikosi chake. Hivyo ameahidi naye kuendelea kufanya marekebisho kadri anavyoendelea kukinoa kikosi hicho, kwani malengo yao ni kutwaa ubingwa msimu huu wa 2022/2023.
Katika mchezo wa pili uliopigwa kwa Mkapa, kati ya Simba na Ihefu ya Mbalali Mbeya; timu ya Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0, bao lililofungwa na Pape Sakho kunako dakika ya 63 na kuufanya mchezo kumalizika kwa matokeo ya 1-0.
Kocha Juma Mgunda baada ya mchezo huo alieleza kuwa mchezo ulikuwa mgumu licha ya ushindi walioupata, na kwamba ligi bado inaushindani mkubwa hivyo yeye na benchi zima la ufundi wanaendelea kupambana ili waweze kutwaa ubingwa kwani mpaka sasa hakuna timu iliyo na uhakika wa moja kwa moja kuwa inatwaa ubingwa. Aliongeza kuwa kikosi chake kimeendelea kuwaptia matokeo chanya licha ya ushindi mfinyu kilioupata bado anaamini kuwa wataendelea kufanya vizuri zaidi kwenye michezo inayofuata.
Naye Juma Mwambusi kocha wa Ihefu alisema kwamba amecheza mechi ngumu tatu mfululizo na kupoteza zote kwa idadi sawa ya goli moja kwenye kila mchezo, lakini anaamini kuwa kila mchezaji wake ameona wapi alipokosea katika michezo iliyopita na namna gani atakwenda kuyafanyia kazi makosa yake. Halikadhalika wao kama benchi la ufundi hawaridhiki na matokeo hayo kwa ujumla hivyo watakwenda kujipanga zaidi ili waweze kushinda michezo inayofuata.
Baada ya matokeo ya Novemba 12, 2022, Azam FC anafikisha alama 23 na kushika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu akiwa mbele mchezo mmoja kwa Simba anayeshika nafasi ya pili (alama 21) akicheza mechi mbili zaidi ya Young Africans anayeshika nafasibya tatu (alama 20).