Azam Veterani na TFF Staff  Wanogesha Siku ya Kuchangia Damu kwa Mechi ya Kirafiki

Mechi kati ya Azam ‘Veterani’ na TFF ‘Staffs’ imepigwa leo katika uwanja wa Azam Complex uliopo Mbagala pembezoni kidogo mwa Jiji la Dar es Salaam ambapo mchezo huo ulikuwa ni wa kirafiki katika kuazimisha siku ya Uchangiaji wa Damu.

Mchezo huo uliopigwa kuanzia majira ya saa 3:00 asubuhi ulikuwa wa kipekee na wa aina yake kufuatia timu zote kusheheni wachezaji wagongwe waliowahi kuzichezea timu mbalimbali hapa nchini.

Kipindi cha kwanza kilianza kwa kasi huku TFF wakionekana kuwa bora zaidi katika dakika 15 za mwanzo, kabla ya  Azam kuamka na kuanza kulishambulia lango la TFF na kufanikiwa kuandika bao la kuongoza mnamo dakika ya 23 huku msumari wa pili ukipigiliwa kunako dakika ya 35 na mchezaji jezi namba 03 na goli la tatu likipachikwa kimyani dakika 42; Mpaka timu zinakwenda kwenye mapumziko Azam ilikuwa ikiongoza kwa bao 3- 0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi kwa upande wa timu ya Azam ambao walionekana kuwa bora zaidi kutokana na maandalizi walioyafanya na hivyo kupelekea kuzitikisa nyavu za timu ya TFF kwa mara ya nne, goli hilo likifungwa katika dakika ya 51 na kuwaacha  Tff wakiwa hoi bin taabani.

Mchezeo huo ulimalizika kwa kwa Azam ‘Veterani’ kuibuka na ushindi mnono wa bao 4 huku kikosi cha Boniface Pawassa kikitoka bila ya kupata walua goli la kufutia machozi.

Kocha wa Azam ‘Veterani’ Zaka Zakazi amesema kuwa mchezo ulikuwa mzuri licha ya kupata matokeo ambayo hawakuyahitaji; kwani wao walitaka kushinda zaidi ya bao tano kutokana na maandalizi waliyoyafanya na ubora wa kikosi chao. Hata kocha huyo amekipiongeza kikosi cha TFF kwa kusema kuwa kimejitahidi kuwazuia wasishidne magoli waliyoyataka.

Naye kocha wa Tima ya TFF Boniface Pawassa amesema kuwa kikosi chake kimeshindwa kufanya vema sana kutokana na wachezaji wake kutofanya mazoezi ya muda mrefu, kwani mazoezi waliyoyafanya yalikuwa ni ya zima moto tu kwa ajili kuazimisha siku ya Uchangiaji wa damu; hivyo amewapongeza wachazaji wake na kuahidi kuwa wataendelea na mazoezi kwa ajili ya kukiweka sawa kikosi hicho kwa ajili ya mechezo mingine.

Mchezo huo ulihudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Ndg. Wallace Karia, ambaye amezipongeza timu zote mbili na kusema kuwaTFF imeunga mkono juhudi hizi za Wizara ya Afya ili kutoa hamasa kwa watu binafsi na taasisi zote kiujumla kushiriki matukio haya muhimu ya kiserikali na kijamii ikiwa ni moja ya njia ya kurudisha kwa jamii na kujenga ushirikiano ulio imara kwa jamii na serikali pia.

Kwa kawaida kila tarehe 14 Juni ni siku maalum ya kuazimisha siku ya wachangia damu duniani kote; hivyo, Wizara ya Afya kupitia kitengo maalum cha damu salama huadhimisha siku hii kwa kutoa elimu juu ya suala zima la uchangiaji wa damu pamoja na kuhamasisha wananchi kuwa na desturi ya kuchangia damu mara kwa mara ili pawepo na damu ya kutosha katika benki ya damu kwa ajili ya kusaidia wahitaji wote.