Balozi Kingu: Tuna imani na timu zetu za taifa
Balozi wa Tanzania nchini Algeria Meja Jenerali Mstaafu Jacob Gideon Kingu amesema serikali bado ina imani kubwa na timu za taifa kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa na kuendelea kuliwakilisha taifa vizuri katika sekta ya michezo.
Hayo ameyasema alipokuwa akizungumza na timu ya taifa ya wanawake Twiga stars pamoja na timu ya wanawake chini ya miaka 20 Tanzanite Queens kuelekea katika michezo mitatu ya kirafiki ya kimataifa ambayo yote itachezwa nchini Algeria.
“Serikali inawatakia kila la kheri katika michezo yenu licha ya kwamba ni ya kirafiki ninahimiza muweke juhudi na muonyeshe ushindani wa hali ya juu ili kujitengenezea mazingira mazuri katika viwango vya FIFA. Niwapongeze sana kwanamna ambavyo mmekuwa mkiiletea nchi ushindi katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, serikali inatambua mchango wenu na itaendelea kuwapa ushirikiano alisema Balozi Kingu.
Naye Kocha mkuu wa timu za taifa za wanawake Bakari Shime alimshukuru Balozi Kingu kwa kufika kuzungumza na wachezaji akisema jambo hilo linawapa wachezaji morali kubwa ya kuendelea kupambana. Kuhusu maandalizi ya michezo kocha Shime alisema maandalizi yote yamekamilika na wachezaji wote wako salama.
Twiga stars itacheza michezo miwili ya kimataifa dhidi ya Algeria Aprili 9, 2023 na mchezo wa pili utapigwa Aprili 11, 2023 wakati Tanzanite Queens wao watacheza mchezo mmoja dhidi ya timu ya wanawake chini ya miaka 20 ya Algeria Aprili 10, 2023. Michezo yote itachezwa katika uwanja wa Nelson Mandela Baraki.