Barka Seif Ajax kwa Mwaka 2021
Mwishoni mwa mwaka 2021 kituo cha Ajax kilichopo nchini Uholanzi kilimtangaza kijana wa kitanzania mwenye umri wa miaka 7 Barka Seif Mpanda kuwa ndio “KINDA BORA WA MWAKA 2021” kutokana na ubora alio uonesha kijana huyo kwa kipindi chote alichokuwa kwenye majaribio ndani ya kituo hicho.
Licha ya umri mdogo alionao kijana Barka, amekuwa akionyesha uwezo mkubwa wa kuumiliki na kuuchezea mpira hali iliyo pelekea Ajax kukubali na kuheshimu kipaji chake na hivyo kumpatia tuzo ya kuwa ndio kijana aliyefanya vyema kwa mwaka 2021.
“Barka alikuwa tofauti na vijana wengine kwa sehemu kubwa, hiyo ndiyo sababu iliyopelekea kuweza kukwatua tuzo mbalimbali. Pia alikuwa ni kipenzi cha wengi kwa kipindi hicho cha wiki mbili za majaribio kwani sit u vituo tu vilivyo vutiwa na uwezo wake bali hata wazazi wa vijana wengine walimpenda sana.” Alisema Hemed mjomba wa Barka ambaye alikuwa naye nchini humo kwa kipindi chote hicho.
Kwa upande wa baba Barka alisema kuwa amefurahi na kufarijika sana kama mzazi kwa kitendo cha kijana wake kuiwakilisha vyema bendera ya Taifa kwenye mataifa mengine, huku akieleza kuwa ni jambo lililo ongeza heshima kwenye familia yake. Zaidi akitaraji mafanikio zaidi kwa kijana wake huyo sambamba na kaka zake wawili ambao pia wanacheza mchezo huo wa mpira wa miguu.
Hakika kijana Barka amekuwa ni moja ya vizazi vilivyoleta faraja na tumaini kubwa Taifa hasa kwa wadau wa soka, hususani wale wanao fahamu kipaji alicho nacho. Vivo hivyo kwa Shirirkisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF ambayo kwa kipindi cha uongozi wa Rais Wallace Karia imekuwa ikiamini sana kwenye Kuibua, Kuvumbua na Kukuza vipaji vya vijana wadogo.