Bashley Express Air cargo mdhamini mpya ligi kuu ya soka la ufukweni

Kampuni ya usafirishaji wa mizigo  Bashley  Express Air cargo imekuwa  kampuni ya kwanza kutoa udhamini kwa ligi kuu ya soka la ufukweni tangu ilipoanza kuchezwa mwaka 2016.

Udhamini huo utadumu kwa muda wa mwaka mmoja ambapo kampuni itatoa jezi seti mbili kwa timu zote 16  zitakazoshiriki ligi ya soka la ufukweni kwa mwaka huu, marekebisho ya uwanja wa kuchezea pamoja na kuwavalisha waamuzi na benchi la ufundi mpaka msimu wa ligi utakapomalizika.

Akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi jezi kwa wawakilishi wa timu Mkurugenzi wa udhibiti na ukaguzi wa TFF Hassan Njama aliwashukuru na kuwapongeza kampuni ya Bashley Express Air cargo kwa uthubutu waliouonyesha wa kudhamini  mchezo wa soka la ufukweni ambao unakua kwa kasi na kutengeneza ajira nyingi kwa vijana.

Naye Mkurugenzi wa Bashley Express Air cargo Mzee Hamad Rashid alisema ” sisi  ni wadau wakubwa wa michezo ni fahari kwetu kuwa sehemu ya kukuza michezo hapa nchini. Tunaamini udhamini wetu katika soka la ufukweni utaleta tija na kuwavutia wadau wengine kuja kudhamini mchezo huu” alisema Mzee Hamad.

Ligi kuu ya soka la ufukweni itaanza Agosti 19, 2023 katika fukwe za Coco, Dar es salaam ikijumuisha timu 16. Michezo hiyo itacheza siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili ya kila wiki