Tanzania yafanikiwa kutinga katika hatua ya fainali michuano ya COSAFA kwa upande wa soka la ufukweni (Beach Soccer) baada ya kupata ushindi mnono dhidi ya Angola hii leo Novemba 19, 2021 katika viwanja vya South Beach, Durban Afrika ya kusini.

 

Tanzania imejihakikishia nafasi ya kuingia katika hatua ya fainali baada ya kupata ushindi wa 4-2 dhidi ya Angola mchezo ambao ulikuwa mzuri sana kwa timu zote mbili magoli ya mapema yaliwatoa mchezoni kabisa wapinzani licha ya kutumia mbinu ya kucheza sana mpira lakini haikuweza kubadilisha matokeo mpaka kipindi cha tatu kinamalizika.

 

Ikumbukwe mchezo uliopita Tanzania ilikutana na Comoros mchezo uliochezwa Novemba 18, 2021 katika viwanja vya south Beach nakumalizika kwa ushindi kwa Tanzania wa goli 2-1 na kuifanya Tanzania kupata nafasi ya kushiriki hatua ya nusu fainali.

 

Baada ya mchezo tulipata maoni kutoka kwa washabiki wa Tanzania waliojitokeza uwanjani kuiunga mkono timu yao akiwemo Yasin Jumanne na kusema “ Tumefurahi sana kwa matokeo haya ni faraja kwetu hapa ughaibuni na watanzania wote cha muhimu tusijisahau tuakikishe tunapambana na tuhakikishe tunashinda magoli mengi sana katika mchezo unaofata” alisema Yasin.

 

Kwa upande wa ufundi Kocha Boniface Pawasa amewapongeza sana wachezaji wake kwa kupambana kuhakikisha wanalinda heshima ya Tanzania na kuwaahidi washabiki na wapenzi wa soka Tanzania ushindi katika mechi ya fainali na kurudi na kombe nchini.

 

Mchezo wa fainali unatarajiwa kuchezwa siku ya jumapili Novemba 20, 2021 katika viwanja vya south Beach vilivyoko Durban, Afrika kusini.