Dodoma Jiji na Biashara United Hakuna Mbabe Jamhuri

Mchezo wa Novemba 21, 2021 uliowakutanisha Dodoma Jiji dhidi ya Biashara United kutoka Mara ulimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu baada ya kufungana bao 1-1 kwenye mchezo uliopigwa majira ya saa moja usiku katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Ni Dodoma Jiji ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 10 tu ya mchezo huo kupitia kwa mshambuliaji wao Annuary Jabir, bao lililodumu mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu hizo kuzidi kuonesha upinzani wa hali ya juu huku zote zikiongeza mashambulizi na kufanya kosa kosa za mara kwa mara. Kunako dakika ya 62 ya mchezo huo timu ya Biashara United ilifanikiwa kupata bao la kusawazisha kupitia mshambuliaji wao machachali aitwae Deogratius Mafie alieyeunganisha krosi safi kutoka kwa David Nkane na kuufanya mchezo huo kukamilika kwa sare ya bao 1-1.

Manahodha wa timu zote waliweza kuzungumza baada ya mchezo huo ambapo maelezo yao yalilandana kwa kiasi kikubwa. Nahodha wa Biashara yeye alidai kuwa mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa kutokana na kila timu kujipanga kwa ajili ya kupata matokeo na kwamba wao kila mchezo wanajipanga vizuri ili kuhakikisha wanamaliza katika nafasi nne za juu kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Naye nahodha wa Dodoma Jiji alisema; kwanza kabisa anamshukuru Mungu kwa kupata matokeo hayo huku akidai kuwa mchezo huo ulikuwa mgumu na wa ushindani kutokana na uhitaji wa alama tatu kwa kila timu; hivyo timu yeyote iliyojipanga vizuri ndiyo inaweza kuibuka na matokeo chanya.

Katika mchezo mwingine wa awali (10:00 jioni) uliowakutanisha KMC FC dhidi ya Azam FC, wenyewe ulimalizika kwa timu ya Azam FC kukubali kipigo cha bao 2-1 kutoka kwa vijana hao wa mjini. Magoli   ya KMC yalifungwa na Matheo Antony kipndi cha kwanza na Salum Kabunda aliyeipatia bao la ushindi timu hiyo kwenye dakika za lala salama. Wakati bao pekee la Azam FC likifungwa na mchezaji Charles Zulu.

Kufuatia matokeo hayo timu ya Dodoma inashika nafasi ya tatu baada ya kufikisha alama 11, alama 3 nyuma ya Simba SC wenye alama 14 huku Young Africans wakisalia kileleni mwa msimamo wa ligi ya NBC na alama zao 16 wakati Biashara United nao wakifikisha alama 8 sawa na  Kagera Sugar.