Bodi ya Ligi (TPLB) Yatoa Ratiba Rasmi ya Ligi Tanzania Bara

Ratiba rasmi ya ligi mbalimbali imetangazwa leo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi Ndg. Almasi Jumapili Kasongo, ligi hizo ni pamoja na Ligi Kuu ‘Vodacom Premier League’ (VPL), ligi daraja la kwanza na ligi daraja la pili.

Hivyo, ligi itaanza rasmi tarehe 13 Juni, 2020 ambapo timu zote zenye viporo ndizo zitakazoanzaa kwa kumalizia viporo vyao ili pawepo na uwiano sawa baina ya timu zote zinazoendelea na ligi.

Timu hizo zenye viporo ni pamoja na Yanga viporo(2), Simba kiporo(1), Azam kiporo(1) Namungo kiporo (1) na Costal Union kiporo (1).

Na atakaefungua mchezo huo wa viporo ni Mwadui FC akivaana na Yanga SC  mchezo utakaochezwa katika kiwanja cha Kambarage mkoani Shinyanga, Coastal Union kukutana na Namungo FC katika uwanja wa Mkwakwani Tanga, Simba SC wao watakuwa mikononi mwa Ruvu Shooting mchezo utakaochezwa uwanja wa Taifa, tarehe 14 Juni, 2020; na atakae kamilisha mzunguko huo wa viporo katika siku hiyo   ni Azam FC  kuvaana na Mbao FC  katika uwanja wa Azam Complex.

Hivyo, baada ya viporo vyote kukamilika ligi itaendelea kama kawaida tarehe 20 Juni, 2020 na kumalizika  Julai, 07-2020.

Pia Kasongo ameainisha kuwa tangu msimu uliopita kulikuwa na ‘play-off’ zinazokutanisha timu za ligi kuu na  timu za ligi daraja la kwanza. Hivyo, mechi hizo zitachezwa kati ya tarehe 29 Julai 2020 ikiwa ni mechi za mwanzo; na tarehe 01 Agosti 2020 (mechi za marudiano).

Kwa minajili hiyo basi, baada ya mechi hizi kukamilika ndipo itakapofahamika ni timu gani iliyopanda daraja na ipi iliyoteremka.

Ligi daraja la kwanza inatarajia kuanza tarehe 19 Juni, 2020 na kumalizika Julai 12, 2020; ligi hii itakuwa na muda mfupi kwa sababu ni  mizunguko minne pekee iliyokua imebaki.

Wakati kwa upande wa ligi daraja la pili yenyewe itaanza tarehe 27 Juni, 2020 na kumalizika Juni, 28 2020 kwa sababu kila timu ilibakisha mchezo mmoja ili kukamilisha hatua ya awali;  hivyo kupata zile timu mbili kutoka kila kundi na kufanya jumla ya timu sita zitakazoelekea katika hatua ya fainali itakayoanza tarehe 10 Julai 2020 hadi  Julai 19, 2020.

Afisa Kasongo aliongeza kwa kusema kuwa katika kukamilisha haya yote, watahakikisha tahadhari zote zinazotolewa na Serekali pamoja na Wizara ya Afya juu ya ugonjwa   Covid-19 zinafuatwa na kuzingatiwa kwa kiwango cha hali ya juu ili kuhakikisha kwamba afya za wachezaji, mashabiki na wadau wa soka  zinakuwa salama salimini.