Mwenyekiti wa Coastal Union ya Tanga Steven Mnguto amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania(TPLB) katika Uchaguzi uliofanyika leo Jumamosi Disemba 1,2018 kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Regal Naivera,Tanga.

Nafasi zilizogombewa katika Uchaguzi huo mdogo ni Mwenyekiti,Mwakilishi wa Klabu za Daraja la Kwanza na Mwakilishi wa Klabu za Daraja la Pili.

Katika nafasi ya Mwenyekiti Steven Mnguto alikuwa Mgombea pekee aliyepigiwa Kura na Klabu za Ligi Kuu.

Katika Kura 18 zilizopigwa Mnguto amepata Kura 16 za Ndio na Kura 2 za Hapana wakati Klabu 2 za Young Africans na African Lyon hazikuwa na muwakilishi.

Kwenye nafasi ya Muwakilishi wa Klabu za Daraja la Kwanza kulikuwa na Wagombea wawili Brown Ernest na Azim Khan Akbar,katika Kura 40 zilizopigwa Brown Ernest amepata Kura 18 na Azim Khan Akbar akipata Kura 22 hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF Malangwe Ally Mchungahela kumtangaza Khan kuwa ameshinda katika nafasi hiyo.

Nafasi ya Muwakilishi wa Klabu za Daraja la Pili ilikuwa na Mgombea mmoja Michael Kadebe katika Kura 40 zilizopigwa Kura 38 zilisema Ndio na Kura 2 zilisema Hapana hivyo Kutangazwa kuwa Muwakilishi wa Klabu za Daraja la Pili.

Baada ya kutangazwa rasmi kuwa Mwenyekiti wa TPLB,Steven Mnguto amewashukuru wapiga Kura wote walioshiriki kwenye Uchaguzi huo mdogo na ameahidi kuwa mtumishi mzuri kwa Klabu pamoja na kulinda maslahi ya Klabu.