Chabruma: Tuna kiu ya kutwaa ubingwa  mashindano ya GIFT

Kocha wa timu ya JKT Queens U-17 Esther Chabruma amesema  ana kiu  ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya CAF ya wasichana chini ya miaka 17 Girls Integrated Football Tournament ‘GIFT’ yanayoendelea nchini Tanzania katika uwanja wa Azam Complex – Chamazi.

Hayo ameyasema mara baada ya mchezo wa Kundi A kumalizika JKT Queens dhidi ya  Elite Jr Academy (Kenya) ambapo JKT Queens iliibuka na ushindi wa goli 2-1 na hivyo kujikusanyia jumla ya alama 6.

Kocha Chabruma alisema, mchezo dhidi ya Elite Jr ulikua ni mchezo mgumu hasa ukizingatia  timu zote mbili ziliingia katika mchezo huo zikiwa zinalingana alama baada ya kupata ushindi katika michezo yao ya kwanza.

” Sikuwa na mpango mwingine zaidi ya kupata ushindi katika mchezo wa Leo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa  wa  mashindano haya. Tuna  deni Kwa watanzania  kwasababu mashindano yanafanyika kwetu hivyo ni lazima tuonyeshe utofauti” alisema Chabruma

Naye Kocha wa Elite Jr Academy FC (Kenya) Cheche Mildred alisema ” mpinzani wangu  aliutawala mchezo katika kipindi cha kwanza, tukajaribu kufanya mabadiliko kadhaa katika kipindi cha pili ambayo nayo hayakuzaa matunda licha ya kwamba tulikua bora katika kipindi hicho”.

Magoli ya JKT Queens yalifungwa na Lydia Kabambo dakika ya 38 na Khadija Petro dakika ya 60.

Mchezo mwingine uliochezwa leo Januari 10, 2023 ulikua ni kati ya  City Lights (Sudani Kusini) na Kenya Academy of Sport (Kenya) na mchezo huo ulimalizika kwa timu ya Kenya Academy kupata ushindi wa goli 5-1 ukiwa ni ushindi wake wa Kwanza baada ya kupoteza katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya JKT Queens.