MCHEZAJI wa timu ya Mbao FC ya Mwanza, Waziri Junior amechaguliwa kuwa mchezaji Bora wa mwezi Novemba wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2019/20, huku Aristica Cioaba wa Azam FC akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Waziri na Cioaba walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa mwezi huo wa Novemba, Mbao ilicheza michezo minne, ikishinda mitatu na kupoteza moja, ambapo iliifunga Coastal Union mabao 2-1 jijini Tanga, ikaifunga Polisi Tanzania bao 1-0 mjini Moshi, ikaifunga KMC mabao 2-0 jijini Mwanza, na ilipoteza kwa bao 1-0 na Azam pia mjini Mwanza.

Kwa mwezi huo Waziri alikuwa na kiwango bora uwanjani, akichangia kwa asilimia kubwa mafanikio hayo ya Mbao, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili, ambapo aliwashinda Obrey Chirwa wa Azam, na Deus Kaseke wa Yanga alioingia nao fainali.

Mbao ilipanda kutoka nafasi ya 14 hadi ya 10 katika msimamo wa ligi inayoshirikisha timu 20.

Kwa upande wa Kaseke alikuwa na mchango mkubwa kwa Yanga akichangia ushindi katika michezo mitatu ambayo Yanga ilicheza na kushinda yote, huku Kaseke akihusika katika pasi za mwisho zilizozaa mabao matatu na kuisaidia Yanga kupanda kutoka nafasi ya 17 hadi ya 12.

Chirwa yeye alitoa mchango mkubwa kwa timu yake ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu ‘hat trick’ wakatiAzam ilipoifunga Alliance mabao 5-0 jijini Mwanza na Azam kwa mwezi huo ilicheza michezo minne ikishinda mitatu na kutoka sare mmoja, hivyo kupanda kutoka nafasiya 13 hadi ya tatu katika msimamo.

Kwa kuwa mchezaji bora, Junior atapata kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka Vodacom Tanzania Plc, na kisimbusi cha Azam Tv wenye haki za matangazo ya Ligi Kuu ya Vodacom.

Kwa upande wa Cioaba aliwashinda Boniface Mkwasa wa Yanga na Hemed Morocco wa Mbao, ambapo Cioaba aliiongoza timu yake katika michezo minne, akishinda mitatu na kutoka sare mmoja, na kupanda kutoka nafasiya 13 hadi ya tatu katika msimamo.

Azam iliifunga Biashara United mabao 2-1 jijini Dar es Salaam, ikaifunga Mbao bao 1-0 na Alliance mabao 5-0 zote ugenini jijini Mwanza na kutoka 0-0 na Kagera Sugar nyumbani, huku Mkwasa akiiongoza Yanga kushinda michezo mitatu iliyocheza ikiifunga Ndanda FC bao 1-0 ugenini mjini Mtwara,
ikashinda nyumbani dhidi ya JKT Tanzania mabao 3-2 na ikaifunga Alliance ugenini mabao 2-1 na kupanda kutoka nafasi ya 17 hadi ya 12.Kwa upande wa Morocco aliiongoza Mbao katika michezo minne, ikishinda mitatu na kupoteza moja, ambapo iliifunga Coastal Union mabao 2-1 jijini Tanga, ikaifunga Polisi Tanzania bao 1-0 mjini Moshi ikaifunga KMC mabao 2-0 jijini Mwanza na ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na Azam pia jijini Mwanza na ilipanda kutoka nafasi ya 14 hadi ya 10.Kwa kushinda tuzo hiyo, Cioaba atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milionimoja) kutoka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)