Dk Maleko Awamwagia Sifa Serengeti Girls
Balozi wa Tanzania Dkt. Jilly Maleko ameipongeza timu ya Taifa ya wasichana wenye umri chini ya miaka 17 baada ya timu hiyo kufanikiwa kuibuka na ushindi wa jumla ya bao 4-0 kwenye mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Urukundo Mjini Ngozi, siku ya Jumamosi ya Aprili 16, 2022 mnamo majira ya saa 9:00 Alasiri kwa saa za Burundi.
Akitoa pongezi hizo katika tafrija fupi iliyoandaliwa kwenye Hoteli ya Bela (Ngozi) kwa ajili ya kupata chakula cha usiku cha pamoja ikiwa kama ishara ya kukubali kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji, benchi la ufundi na viongozi walioambatana na timu hiyo ya Serengeti Girls, Balozi Maleko alisema kuwa vijana wanafanya kazi kubwa yenye kuiheshimisha nchi akisema yeye akiwa mwakilishi wa Rais Samia Suluhu Hassan amefarijika sana kwa jinsi timu inavyo pambana kwa ajili ya kuendelea kupeperusha vyema Bendera ya Tanzania.
Balozi Dk Maleko aliongeza kuwa anatambua kazi inayofanywa na wachezaji, walimu na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakiongozwa na Rais Wallace Karia, kwani wamekuwa wakiitangaza vizuri nchi kwa kuleta ushindi hasa wasichana ambapo aliahidi kufikisha pongezi hizo kwa Rais Samia kuwa naye ni mdau mkubwa wa soka la wanawake.
Aidha, Balozi huyo aliimwagia Serengeti Girls kila aina ya sifa akiweka bayana kuwa serikali inayoongoza na Mama Samia itaendelea kutoa sapoti ili kuzidi kutatua changamoto zinazowakibili wachezaji wa kike wakati na baada ya kustaafu kucheza soka.
Akihitimisha hotuba yake fupi, Balozi Dk Maleko aliitakia timu ya Serengeti Girls kila la kheri kuelekea mchezo wao wa marudiano utakaochezwa Siku ya Mei Mosi huko Visiwani Zanzibar pamoja na ile itakayofuata baada ya timu hiyo kuvuka hatua hiyo ili iweze kutinga Kombe la Dunia.
Naye Mbunge wa Viti Maalum kutoka Tanga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia huduma za jamii, Bi.Husna J. Sekiboko aliahidi kuzichukua changamoto zinazowakibili wachezaji hao na kuzipeleka Bungeni ili zikafanyiwe kazi kwani Bunge ndio chombo kikubwa kinachoishauri serikali; hivyo ameahidi kwenda kupigania uboreshwaji wa mazingira ya timu zote za wanawake pamoja za wanaume pia.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) Abdullatif Said Yassin alisisitiza uboreshaji wa mazingira ya mpira kwa wasichana hao na timu zote. Alieleza mpira ni ajira kama zilivyo kazi nyingine hivyo atakwenda kushauriana na Rais wa TFF, Wallace Karia ili kwa pamoja waweze kuongeza nguvu zaidi katika kuhakikisha mpira unazidi kuleta tija kwa vijana wa Tanzania.
Kocha Mkuu Bakari Shime, alitoa shukrani kwa Balozi akisema kuwa wamesafiri safari nyingi lakini safari hiyo imekuwa ya kipekee kutokana na uwepo wa viongozi wengi waliokwenda kuwatia moyo, japokuwa uwepo wa viongozi hao pia ulikuwa ni mtihani kwao kwani iliwalazimu kutafuta ushindi kwa kila hali ili kuwapoza kwa safari ndefu, huku nahodha wa kikosi hicho Noela Luhala akiwakikishia Watanzania kuendelea kuipigania nchi kwa hali na mali wakiwa na lengo moja la kuipeleka Tanzania kwenye Kombe la Dunia ifikapo Oktoba, mwaka huu.
Akitoa neno la shukrani kwa Balozi Maleko, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF,Mwl. Salum Madadi alisema hakika wamefarijika sana kuona serikali inawaunga mkono hivyo wao kama Shirikisho linalosimamia soka nchini watazidi kubuni mikakati mbalimbali ili kuendelea kuipeperusha vyema Bendera ya nchi kupitia mpira wa miguu.