Dkt. Samia Kuendelea Kununua Magori Kimataifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ataendelea kutoa motisha kwa timu zote zinazoshiriki michuano ya Kimataifa ya CAF kwa kununua kila goli (2023/2024) kama ilivyokuwa kwenye msimu ulimalizika wa 2022/2023.

Mhe. Rais Samia aliyasema hayo Agosti 06, 2023 kwenye Tamasha la “Simba Day” ambapo aliupongeza pia uongozi wa klabu ya Simba kwa maandalizi mazuri ya siku yao ambayo ilikuwa Maalum kwa ajili ya kutambulisha wachezaji wao watakao kuwa katika kikosi cha msimu mpya.

Akihutubia maelfu ya mashabiki waliojitokeza kuisapoti timu hiyo ya Kariakoo (DSM), Rais Samia alisema kuwa ataendelea na utaratibu wa kununua kila goli litakalopatikana ikiwa ni sehemu ya kuchagiza mafanikio kwa timu shiriki kwenye Michuano hiyo ya Kimataifa ambayo Simba SC, Young Africans SC, Azam FC na Singida Fountain Gate zitashiriki msimu ujao.

Mbali na Ahadi hiyo Mhe. Rais alisema kuwa anahitaji kuona mafanikio yaliyofikiwa na Young Africans SC msimu uliopita yanaenda kupatikana tena kwa timu zote na kwamba itapendeza zaidi endapo timu hizo zikipita hapo ili kuendelea kuliletea heshma Taifa kupitia michezo, hususani Mpira wa Miguu.

Rais Samia aliendelea kumwaga pongezi zake kwa viongozi wa klabu hiyo kongwe nchini, akisema kuwa Simba imefanya jambo kubwa na la kuigwa baada ya kupeleka Kibegi kwenye Mlima Kilimanjaro, jambo ambalo limeunga mkono dhana yake ya kuwavutia watalii kupitia Filamu ya “Royal Tour”ambayo imeongeza Utalii kwa kiwango kikubwa nchini.

Aidha, Mhe. Rais Samia alibayanisha Mipango madhubuti ya Serikali anayoiongoza kuwa Serikali yake imekusudia kujenga viwanja viwili Dodoma na Arusha vitakavyokuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki yapata elfu 30 Kila kimoja.

Alisema Serikali imechukua hatua hiyo kufutia ombi lilitolewa na nchi tatu Tanzania Kenya na Uganda la kuwa mwenyeji wa AFCON za 2027. Hivyo, kwa kutambua mchango wa michezo katika kukuza uchumi na kutengeneza ajira kwa vijana nchini, Serikali imeamua kuboresha miundo mbinu ya viwanja hivyo pamoja na kuufanyka ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mhe. Rais Samia katika tukio hilo aliambatana na viongozi Serikali na mpira pia ambapo kwa upande wa Serikali alikuwa ni Waziri wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Pindi Chana, Mkuu wa Mkoa   wa Dar es Salaam Mhe.Albert Chamalamila na wengine wengi, huku viongozi wa mpira wakiongozwa na Rais wa TFF. Wakati huo kwa upande wa waandaaji wa Tamasha hilo Simba alikuwepo Rais wa heshma Mohammed Dewji “Mo”, Mwenyekiti Wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Salum Abdallah “Try Again” Mtendaji Mkuu wa Simba (CEO)  Imani Kajula, Mwenyekiti wa Simba Murtaza Mangungu na wengine wengi.

Tamasha hilo la Simba lilihitimishwa kwa  mchezo wa kirafiki kupigwa kati ya Simba na Power Dynamo kutoka Zambia ambapo Simba ilishinda bao 2-0.