Dodoma jiji Kuifuata Kagera Sugar Fainali U20

Timu ya vijana U20 ya Dodoma jiji inayoshiriki ligi kuu (NBC U20 Premier League) imefanikiwa kutinga hatua ya fainali baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Azam FC Mei 23, 2024 uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Mchezo huo ulioamuliwa Kwa mikwaju ya penati ulimalizika kwa dakika 120 bila timu yoyote kuona lango la timu pinzani, licha ya Azam FC kuonekana kuwa bora zaidi Kwa kutengeneza mashambulizi mengi zaidi.

Penati 5 walizopata Dodoma Jiji dhidi ya panati 3 za Azam FC ndizo zilizoamuwa matokeo ya mchezo huo, hivyo Kwa matokeo hayo Dodoma Jiji itacheza Fainali na Kagera Sugar wakati Azam FC ikipiga hesabu za kukutana na Simba SC kutafuta mshindi wa tatu.

Akizungumza baada ya mchezo huo kocha wa Dodoma jiji aliwapongeza vijana wake Kwa kujituma na kufanikisha timu hiyo kufikia fainali, huku aliwapongeza pia Azam FC kwa kuwa bora zaidi licha ya timu yake kupata matokeo.

Wakati Kwa upande wa Azam FC kocha Mohamed Badru alisema matokeo ya mchezo huo licha ya kutokuwa upande wao lakini aliwapongeza vijana wake kwa kupambana wakati wote, huku akisema kwamba bado anakibarua na kuwatia moyo wa kupambana kwenye mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.

Michezo ya mwisho inatarajiwa kuchezwa Juni 2, 2024 uwanja wa Azam Complex Chamazi ambapo pia sambamba na mechi hizo za fainali na kutafuta mshindi wa tatu pia sherehe za ubingwa zitafanyika Uwanjani hapo.