Leo ni siku ya fainali ya michuano ya COPA DAR ES SALAAM iliyoanza Disemba 22 ambapo timu kutoka nchi 5 (Burundi, Malawi, Seychelles, Tanzania na Uganda) zimekuwa zikimenyana vikali katika viwanja vya COCO BEACH Oystabey  Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Michuano hiyo inafikisha siku tano hii leo na kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo ndio siku ya mwisho ambayo itatoa bingwa wa michuano hiyo.

Mechi kali na ambayo macho na masikio ya wengi waliokuwa wakifuatilia michuano hii inatarajiwa kuwa ni ile inayowakutanisha Burundi dhidi ya Tanzania ambao wote wamejikuta tu wamelingana pointi na magoli pia ambapo timu zote zina jumla ya pointi sita na magoli 17 baada ya kucheza mechi tatu kwa kila timu.

Mshindi katika mchezo huo wa leo kati ya Burundi na Tanzania ndio utatoa bingwa wa mashindano hayo ya COPA DAR ES SALAAM kwa kuwa atakee shinda atakuwa na alama tisa ambazo hakuna timu inayoweza kufikia miongoni mwa zile zinazotarajia kuingia uwanjani leo baada ya muda mfupi ujao.

Kabla ya mechi ye leo Tanzania imecheza michezo mitatu ikiwa na pointi sita sawa na Burundi, wakifuatiwa na Seychelles  iliyomaliza michezo nyake yote (4) na kujikusanyia alama tano, alama moja  juu ya Uganda yenye alama nne huku Malawi wakiburuza mkia pasipo alama yeyote.

Endapo Uganda ikishinda mechi ya leo basi itafikisha alama saba; ambazo zinaweza kulingana pia na mshindi atakeye patikana kwa mikwaju ya penati ambapo kwa sheria za mchezo wa soka la ufukweni mshindi kwa njia ya penati hupata alama moja tu.

Mechi ya utangulizi  itakuwa kati ya Uganda na Malawi ambapo Uganda atakuwa na kibarua kikubwa kwa sababu anakutana na timu ambayo haina alama hata moja.

Mratibu wa Soka la Ufukweni Jonathan Kassano anasema kuwa mashindano hayo yameendeshwa kwa mfumo wa ligi lakini baada ya timu za Tanzania na Burundi kufungana alama na magoli huku zikikutana katika mchezo wa mwisho ndio zimetengeneza fainali.

Kassano ameeleza kuwa mshindi wa kwanza  katika mashindano hayo atapata kikombe na medali ya dhahabu, mshindi wa pili atapata medali za shaba huku mshindi wa tatu akipewa medali ya ‘silva’.

Mgeni rasmi katika fainali hizi atakuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo; Ally Posi.

Mchezo wa kwanza kati ya Malawi na Uganda unatarajiwa kuanza saa tisa kamili Alasili, huku ule wa fainali kati ya Burundi na Tanzania ukitarajiwa kupigwa majira ya saa kumi jioni.