Fainali Mwanga City Dhidi ya Gets Programm WRCL

Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kwa Wanawake inayoendelea kutimua vumbi jijini Mwanza imemaliza hatua ya nusu fainali ambapo timu nne zilizofuzu kwenye hatua hiyo zote zimeishacheza mechi zake, huku washindi wa michezo miwili ya nusu fainali Gets Programm na Mwanga City Queens wakitarajia kukutana kwenye hatua ya fainali Julai 27, 2023.

Michezo hiyo ya nusu fainali iliyopigwa Julai 25, 2023 kwenye uwanja wa Nyamagana ambapo mchezo wa kwanza uliochezwa majira ya saa 7:30 mchana ukiwakutanisha Sayari Woman dhidi ya Mwanga City Queens huku mchezo mwingine ukipigwa mnamo majira ya saa 10:00 jioni ukiwakutanisha Mpaju Queens kutoka Mbeya dhidi ya Gets Programm ya Dodoma.

michezo hiyo miwili ilimalizika kwa timu za Mwanga City (Kigoma) na Gets Programm (Dodoma) kupata ushindi, unao wafanya wawili hao kukutana katika fainali kusaka Bingwa wa Mashindano hayo ya mabingwa Wa Mikoa kwa Wanawake.

Hata hivyo mchezo wa nusu fainali ya kwanza uliopigwa kati ya Gets Programm na Mpaju Queens ulimalizika kwa timu hizo kutokufungana ndani ya dakika 90, mpaka Gets ilipopata ushindi wa magoli 2-0 baada ya dakika 30 zilipoongezwa ili kufikisha dakika 120 ambazo kikanuni huongezwa kama hajapatikana mshindi ndani ya dakika 90 hasa katika hatua ya nusu fainali na fainali.

Kwa upande wa mchezo mwingine ule wa jioni, Mwanga City waliifunga Sayari Woman magoli 2-1, matokeo yaliyopatikana ndani ya dakika 90.

Fainali itapigwa Julai 27, 2023 kwenye uwanja wa Nyamagana, ambapo pia mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya Mpaju Queens (Mbeya) na Sayari Woman (Dar es Salaam) utapigwa siku hiyo ya Alhamis kama wa utangulizi kabla ya fainali hiyo.