Fountain Gate Academy yatwaa ubingwa CECAFA U-15
Shule ya Fountain Gate Academy (Dodoma) imetwaa ubingwa wa mashindano ya CAF Kwa shule za msingi na sekondari ukanda wa CECAFA kwa upande wa wasichana baada ya kuifunga timu ya Awaro SS ya Ethiopia goli 3-0 katika mchezo wa fainali.
Mashindano hayo yamemalizika leo Februari 19,2023 katika uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es salaam.
Magoli matatu ya Fountain Gate yalifugwa na Mary Aron Siyame, Rede Julius Boniphace pamoja na Winifrida Hubert ambaye aliibuka kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo huku mchezaji Zainabu Dotto Karuka akibeba tuzo ya mchezaji Bora.
Akizungumza baada ya mashindano kumalizika Rais wa TFF Wallace Karia aliwapongeza Fountain Gate Academy kwa kutwaa ubingwa na kuongeza kuwa TFF itaendelea kutoa ushirikiano wa hali na Mali ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mashindano yajayo”.
Naye mmiliki wa shule za Fountain Gate Japheth Makau alisema ” hakika vijana wamepambana na wanastahili pongezi kubwa, shule za Fountain Gate zitaendelea kuibua na kukuza vipaji vya vijana katika soka ili kuwepo na vijana watakaoleta mabadiliko katika soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla”.
Royal Giant ya Uganda nayo iliibuka bingwa wa mashindano Kwa upande wa wavulana huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Geda Roble ya Ethiopia na nafasi ya tatu ikibebwa na Libya PS ya Sudani Kusini.
Mgeni rasmi katika fainali za CECAFA U-15 alikua Waziri wa sanaa utamaduni na michezo Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana aliyeambatana na katibu mkuu wa wizara hiyo Said Yakubu pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa idara ya maendelezo ya michezo Ally Mayay. Viongozi wa mashirikisho mbalimbali ya mpira wa miguu nao walihudhuria.