Fredy Mbuna: Lengo la ubingwa bado tunalo

Kocha msaidizi wa timu ya Yanga Princess Fredy Mbuna ametuma salamu kwa wapinzani wao Simba Queens kuelekea katika  ‘derby’ ya kariakoo itayopingwa Machi 22, 2023 katika uwanja wa Uhuru, Dar es salaam akisema lengo la kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya wanawake  bado wanalo hivyo  Simba Queens wajipange.

Hayo ameyasema alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  kuelekea katika mchezo huo wa ligi kuu ya wanawake ambapo alisisitiza kwamba kikosi chake kimejiandaa vizuri kuhakikisha kinapata matokeo mbele ya Simba Queens licha ya kukiri kutokufanya vizuri katika mechi 2 za mwisho ambapo kilipoteza mbele ya Fountain Gate Princess na kutoka sare mbele ya Mkwawa Queens.

” Ni kweli hatujawa na matokeo mazuri katika mechi za hivi karibuni lakini bado tuna imani ya kubeba alama tatu kwa Simba Queens. Uzito wa dabi tunaujua na hatutoruhusu kupoteza kirahisi na kuwataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu Yao. alisema kocha Mbuna

Naye Charles Lukula kocha  mkuu wa Simba Queens alisema  maandalizi yote yamekamilika, wachezaji wote wako vizuri tayari kwa mchezo na hakuna mchezaji yoyote atakayemkosa katika mechi ya kesho. Kupata ubingwa sio kazi kazi ni kutetea ubingwa na sisi Simba Queens tutapambana mpaka mwisho.

Yanga Princess ambaye ni mwenyeji wa mchezo anashuka dimbani akiwa nafasi ya 4 katika msimamo wa ligi kuu ya wanawake  akiwa na jumla ya alama 21 katika michezo 11 ambayo tayari imecheza , wakati  Simba Queens yeye akiwa kinara wa Ligi hiyo Kwa jumla ya alama 26.