Geita Gold Yabanwa Mbavu Jiooni Ikiwa Uwanja wa Nyumbani
Mchezo uliopigwa Disemba 04, 2022 majira ya saa 10:00 kwenye dimba la Geita, kati ya wenyeji Geita Gold na Mtibwa Sugar ulimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu kwa kufungana bao 2-2.
Katika mchezo huo timu zote zilikuwa na moto zikipambana kutafuta kumaliza duru ya kwanza kwa kuvuna lama tatu, lakini mpaka dakika zinatamatika hakuna aliyeweza kuibuka na lama zote tatu, baadala yake wawili hao waliambulia alama moja moja.
Ni Mtibwa Sugar ndiyo aliyetangulia kuandika bao la kuongoza katika dakika ya 10 ya mchezo kupitia kwa Juma Nyangi huku Geita Gold wakijibu mapigo kunako dakika ya 35 ya mchezo kupitia kwa Saidi Ntibazonkiza aliyekwamisha kimiani mkwaju wa penati na kuzifanya timu hizo kwenda kwenye mapumziko ubao ukisoma 1-1.
Kipindi cha pili Geita Gold waliuanza mchezo kwa kasi zaidi na kufanikiwa kuandika bao la pili kunako dakika ya 49 kupitia kwa Juma Liuzio, bao hilo likisawazishwa na Mtibwa Sugar jioni kunako dakika ya 90+ ambapo mchezaji wa Geita Gold, George Wawa.
Fred Felix Minziro kocha Mkuu wa Geita Gold alisema kuwa timu yake imepambana vilivyo lakini mwishoni wamefanya makosa ambayo yaliwanufaisha Mtibwa Sugar huku kocha Mkuu wa Mtibwa Salum Mayanga naye akisema matokeo hayo kwake yana ahweni kuliko kupoteza alama zote. Aliongeza akisema ligi ya mwaka huu ni ngumu kwa kuwa kila timu inasaka kufanya vizuri hivyo haikuwa rahisi kupata alama hiyo moja.
Mchezo huo unazifanya timu hizo kufikisha alama 22 kila moja huku zikitofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa jambo ambalo linaipatia faida zaidi Geita Gold ambayo inasalia katika nafasi ya 5 wakati Mtibwa wao wanashika nafasi ya sita, wakisubiri timu nyingine zikamilishe ratiba ili kujua ipi inakuwa wapi baada ya michezo 15 kukamilika kwa timu zote za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Katika mchezo huo kiungo mshambuliaji kutoka Bujumbura Saidi Ntibazonkiza hakuweza kumaliza dakika 90 baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwa kumchezea faulo mchezaji wa Mtibwa Sugar.