Gets Programm Bingwa WRCL

Timu ya Gets Programm imefanikiwa kubeba ubingwa kwenye ligi ya Mabingwa wa mikoa kwa wanawake iliyofanyika jijini Mwanza baada ya kuifunga timu ya Mwanga City kwenye mchezo wa fainali ulio malizika kwa Gets kupata ushindi wa goli 1-0.

Mchezo huo uliopigwa Julai 27, 2023 kwenye uwanja wa Nyamagana majira ya saa 10:00 jioni ulianza kwa kuonekana mgumu pande zote, huku kila timu ikishambulia kila inapopata nafasi hata kufanya kipindi cha kwanza timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana.

Kipindi cha pili kocha mkuu wa Gets Programm (Dodoma) aliamua kufanya mabadiliko ya kumtoa mchezaji Millan Maron, sambamba na kumtambulisha mchezoni Eva Saddy aliyeifungoa timu yake bao pekee la ushindi Eva Saddy zikipata ushindi and kufanya timu hiyo kubeba ubingwa mbele ya Mwanga City.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika kocha Aristides Innocent alisema kuwa mashindano yalikuwa mazuri kutokana na ushindani wa kila timu hasa zile zilizofika hatua ya robo fainali na kuendelea. Sambamba na kuwasifu wachezaji wake kwa kufuata maelekezo wanayopatiwa kila wanapokuwa mchezoni.

Kwa upande wa kocha wa Mwanga City Kashinde Mangapi mwenyewe alisema mashindano hayakuwa mepesi na kwamba kila timu iliyofika hatua ya fainali ilikuwa bora hasa katika maandalizi. Kocha huyo pia amewapongeza wachezaji wake na timu pinzani kwa mechi bora na yenye mvuto.

Mchezo mwingine uliochezwa kabla ya fainali ulikuwa wa kutafuta mshindi wa tatu ambapo timu ya Mpaju Queens (Mbeya) ilimaliza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sayari Woman (Dar es Salaam),matokeo yaliyofanya Mpaju kushika nafasi ya tatu.

Hata hivyo tuzo mbalimbali pia ziligawiwa kwenye mashindano hayo ikiwemo ya timu yenye nidhamu iliyokwenda kwenye timu ya Chipuputa Queens (Mtwara). Tuzo nyingine ni Mchezaji bora: Beatrice Charles, Kipa bora: Habi Faida na Mfungaji bora Irene Chitanda (magoli 13).