TFF Yazidi Kupata Wadhamini wa Ligi Kuu Bara
Ligi Kuu ya NBC Tanzania imezidi kupata neema baada ya kupatikana kwa mdhamini mwingine “GSM GROUP”aliyesaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya fedha za Kitanzania kiasi cha shilingi Bilioni Mbili nukta moja (2,100,000,000) kwa ajili ya kuwa mdhamini mweza wa ligi hiyo inayoshika nafasi ya nane kwa ubora Afrika ambayo kwa sasa inadhaminiwa na NBC.
Mkataba huo baina ya GSM GROUP na TFF, ulisainiwa Novemba 23, 2021 katika Hoteli ya Serena iliyopo Jijini Dar es Salaam ambapo pande zote mbili ziliwekeana saini. Saini hizo ziliwekwa kupitia wawakilishi wa pande zote mbili; kwa upande wa GSM uliwakilishwa na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM Eng. Hersi Said, huku kwa upande wa TFF ukiwakilishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF Athumani Nyamlani.
Akizungumza kwa niaba ya Makampuni ya GSM GROUP, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM GROUP, alisema kuwa GSM wameamua kuwekeza kiasi hicho cha fedha kutokana na kuridhishwa na uongozi uliopo TFF unaoongozwa na Rais Wallace Karia ambao unaonesha usimamizi mzuri wenye kutoa mwelekeo sahihi wa kukuza soka la Tanzania. Hata hivyo, Hersi aliongeza kuwa udhimini huo pia ni moja ya mikakati iliyopo katika kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyo chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imeonesha kuithamini michezo kwa ujumla.
Kufuatia jitahada hizo za kuinga Serikali na TFF zinazofanywa na wadau mbalimbali, GSM nayo pia imeona kuwa iko haja ya kuongeza nguvu katika kuidhamini ligi hiyo ambayo mdhamini wake Mkuu ni NBC. Lengo kubwa la kufanya hivyo ikiwa ni kuendelea kutoa fursa kwa vijana kunufaika na vipaji walivyonavyo katika soka; huku shabaha nyingine ikiwa ni kuimarisha ushindani ambao utawezesha upatikanaji wa timu bora za Taifa; kwani timu bora za Taifa haziwezi kupatikana pasipokuwa na ligi imara na bora pia.
Akitoa shukurani kwa niaba ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani aliwashukuru GSM kwa kuona umuhimu mkubwa wa kuiunga mkono TFF pamoja na TPLB hali kadhalika Serikali katika kuendeleza mpira wa miguu nchini. Kwa minajili hiyo, TFF nayo haina budi kuwaunga mkono kwa kuwapatia ushirikiano wa kutosha GSM kwa kufanya nao kazi vizuri ili kuhakikisha mpira wa Tanzania unazidi kukua na kwenda mbali zaidi kwa faida ya leo na kesho.
Alisema kuwa fedha zinazotolewa na wadhamini hazitolewi hivi hivi, bali ni kutokana na utekelezaji mzuri pamoja na usimamizi madhubuti unaofanywa na TFF na TPLB, ambapo fedha hizo huelekezwa moja kwa moja kwenye matumizi sahihi yanayogusa maslahi mapana ya vilabu pamoja na maendeleo ya vilabu na timu husika. Aliongeza kwa kusema kuwa sasa hivi TFF na Bodi ya Ligi hawataki kusikia wala kuona timu inafungwa au kushindwa kusafiri kwa sababu ya kukosa fedha za huduma muhimu kwa timu; hivyo watahakiksha fedha hizo zinakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo.
Makamu huyo wa Rais alieleza bayana kuwa hapo awali vilabu vilikuwa vikipata taabu katika kusafirisha timu zao, kupata BIMA pamoja na kuwalipa wachezaji wao mishara kwa wakati, ambapo ilifikia kiasi cha wachezaji kupitisha hata miezi mitatu pasipo kupata pesa; halikadhalika na makocha hasa kwenye vilabu ambavyo vilikuwa havina wadhamini binafsi kama ilivyo kwa baadhi ya vilabu vikubwa vya Young Africans, Simba SC na Azam FC.
Aliendelea kusema kuwa hali hiyo ilizidi kuwa mbaya hadi kufikia wakati timu yenye uwezo inaingia gharama ya kuilipia gharama timu nyingine na kuishawishi iweze kukabli kuchezea eneo fulani mchezo wake wa nyumbani; na kwa kuwa timu hiyo haina uwezo basi ilikuwa vigumu kukataa isipokuwa kukubaliana na matakwa ya mpinzini wake amabaye pia aligeuka kuwa mdhamini wa muda. Hii ilipelekea kupunguza ari ya timu hiyo kupambana, jambo ambalo lilikuwa linapunguza ushindani kwa baadhi ya timu kutokana na mazingira hayo.
Baada ya udhamini huo wa GSM na NBC, ligi hiyo kwa upande wa haki za matangazo ya Televisheni inadhaminiwa na Azam Media Ltd. huku TBC nao wakiwa wameingia mkataba wa matangazo ya redio. Kupitia udhamini huo unaowekwa na wawekezaji hao wote, sasa ni dhahiri kuwa Ligi ya Tanzania inaendelea kukua na kuongeza thamani kila uchao.
Hafla hiyo fupi ya kutia saini kwa pande zote mbili ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi kama vile; Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF Athumani Nyamlani, Makamu wa Pili wa Rais wa TFF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Steven Mnguto, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB Almasi J. Kasongo, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Eng. Heris Said, Mkurungenzi wa Ukaguzi wa Ndani wa TFF, Mkurugenzi wa Sheria Habari na Masoko wa TFF Boniface Wambura, Wanasharia wa pande zote mbili pamoja na viongozi mbalimbali wa vilabu.