Hali ya Hewa Imeigharimu Timu

Timu ya Taifa ya wasichana chini ya miaka 20 Tanzanite imeshindwa kuendelea na safari ya kuwania tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia 2022, mara baada ya kupoteza katika mchezo wake wa marudiano dhidi ya Ethiopia Februali 04, 2022.

Mchezo huo uliomalizika kwa Tanzanite kupoteza kwa mabao 2-0 ulichezwa huko nchini Ethiopia kwenye uwanja wa Abebe Bikila majira ya saa 10:00 jioni kwa majira ya saa za Afrika Mashariki, huku Tanzanite wakionekana kupambana kutetea nafasi yao ya kuongoza mara baada ya ushindi wa bao 1-0 waliopata kwenye mchezo wa awali.

Licha ya hali ya hewa kuwa si rafiki kwa wachezaji wa kikosi cha Tanzanite, bado walionekana kupambana kwa takribani vipindi vyote viwili hasa katika kipindi cha kwanza  kabla ya kuruhusu bao la kwanza lililofungwa mnamo dakika ya 35. Na goli la pili lilifungwa dakika ya 80.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika kocha mkuu wa Tanzanite Bakari Shime alieleza kuwa hali ya hewa ndio sababu kubwa iliyopelekea kikosi chake kupoteza mchezo licha ya kuonekana kikipambana kwa takribani dakika zote za mchezo.

“Tumepoteza nafasi nyingi za kufunga magoli, pengine ni kupoteza umakini kwa wachezaji au pengine kukosekana kwa utulivu. Kwa ujumla tumejifunza vitu vingi husasini kuendana na hali ya hewa pamoja na ambavyo ingetubidi kuweka nguvu kubwa kwenye mchezo wetu wa awali ingesaidia kutubeba kama tungekuwa na hazina kubwa ya Magoli kabla ya mchezo wa marudiano”. KAULI YA BAKARI SHIME

Timu ya Tanzanite tayari imewasili nchini Februali 05, 2022 ambapo pia alizungumza Katibu mkuu wa TFF Kidao Wilfred “ Kwa maandalizi tuliyafanya kwenye timu yetu, hatukutegemea matokeo haya lakini pia tumejifunza mengi hasa katika mashindano ya namna hii ya mtoano ni jinsi gani yanapaswa kuwa.” Alisema Katibu mkuu

Hata hivyo alieleza kuhusiana na mashindano yaliyo mbele kwa timu ya Taifa ya wasichana chini ya miaka 17 ambao pia wengi wao wapo kwenye timu hiyo ya Tanzanite kwamba kupitia mashindano hayo wanaamini wachezaji wameweza kujifunza baadhi ya vitu muhimu hasa kuweka nguvu zaidi kwenye michezo yote ya nyumbani.

Tanzanite imeondolewa kwenye mashidano hayo kwa upande wa timu za Afrika zilizo fanikiwa kufika  mpaka katika hatua hiyo ya nne, hatua inayofuata Ethiopia atakutana na kati ya timu ya Ghana au Uganda.