Hemed Morocco:Tumejiandaa kuwapa Furaha watanzania
Kocha msaidizi wa timu ya Taifa Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema Taifa Stars imejipanga kuwapa furaha watanzania katika mchezo wa marudiano wa kufuzu AFCON dhidi ya timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ utakaopigwa Jumanne Machi 28,2023 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam majira ya sa 2:00 usiku.
Akizungumza na wanahabari kuelekea katika mchezo huo kocha Morocco alisema, maandalizi yote yamekamilika na wachezaji wote wako vizuri hakuna majeruhi yoyote mpaka sasa. Wachezaji Wana morali kubwa na wamejipanga kuwapa Furaha watanzania wote.
” Tunafahamu ugumu wa mechi dhidi ya Uganda hivyo tunakwenda kupambana, ubora wa kikosi umeonekana ndiomana tulipata matokeo ugenini lakini tunaamini ongezeko la Shomari Kapombe na Mohammed Hussein litaongeza nguvu katika kikosi kutokana na uwezo na uzoefu walionao”. Alisema kocha Morocco
Kocha mkuu wa Uganda ‘The Cranes’ Milutin Sredojevic ‘Micho’ alisema ” hakuna timu isiyo na mapungufu duniani kila timu inakosea sisi tulikosea Tanzania ikatuadhibu. Tumerekebisha makosa yetu na nina imani tutashinda.Tunacheza na timu nzuri ambayo ligi yake inafanya vizuri Afrika lakini pia ina wachezaji wanaofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa kama klabu bingwa Afrika na kombe la shirikisho Afrika, ushindani ni mkubwa lakini tumejiandaa kubeba alama tatu.
Simon Msuva naye akiongea kwa niaba ya wachezaji wenzake aliwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwaunga mkono huku akiahidi ushindi katika mchezo huo wakati Nahodha wa Uganda Emmanuel Okwi akisema kuna uzito mkubwa wa kuvaa jezi ya taifa, kila mchezaji anafahamu majukumu yake tupo hapa kwa ajili ya kupambana.
Mchezo wa mkondo wa Kwanza Tanzania ilibeba alama tatu katika uwanja wa Suez Canal, Misri goli pekee likifungwa na Simon Msuva Dk ya 68 na kuifanya Tanzania kushikilia nafasi ya pili ikiwa na alama nne wakati mpinzani wake Uganda akiwa nafasi ya mwisho na alama moja katika msimamo wa kundi F.