Ihefu Yaivurugia Hesabu Young Africans
Timu ya Ihefu imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya vinara wa Ligi Kuu ya NBC Young Africans baada ya kuichapa timu hiyo ilipoialika kwenye uwanja wa nyumbani wa Highland Estates uliopo Mbalali Jijini Mbeya.
Mechi hiyo iliyochezwa Novemba 29, 2022 majira ya saa 10:00 jioni ilianza bila kasi kubwa hasa kwa upande wa Young Africans ambao waliingia kwa kujiamini kutokna na kuwa na rekodi ya kucheza mechi 49 za ligi ya NBC pasipo kupoteza hata mchezo mmoja, hali iliyowafanya wapinzani wao Ihefu kuwa hamu ya kupata matokeo katika mchezo huo.
Young Africans walitangulia kupata bao la mapema mnamo dakika ya 8 kupitia kwa kiungo kiraka Yannick Bangala aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na Joyce Litombo Lomalisa, bao ambalo halikudumu kwa muda mrefu kabla ya Ihefu kusawazisha bao hilo kunako dakika ya 38 kupitia kwa Never Tigere aliyepiga mpira wa kufa uliomshinda Djigui Diarra na kutinga nyavuni.
Wakati Young Africans wakiwa katika harakati ya kusaka bao la pili Ihefu walifanya shambulizi lililopelekea kona iliyozaa bao la pili lililofungwa na Lenny Kissu mnamo dakika ya 62 na kuiacha timu ya wananchi ikipigwa na butwaa kwa kutoamini kilichotokea kwani bao hilo lilidumu mapaka kipyenga cha mwisho cha mwamuzi.
Matokeo hayo yanaifanya Ihefu kuutafuna mfupa uliowashinda wengi na hivyo kuiharibu rekodi ya Young Africans ya kutaka kufikisha michezo 50 pasipo kupoteza mchezo ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na wapenzi na wadau wa soka pia.
Baada ya mchezo huo kocha wa Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi alisema uchovu ndiyo uliwafanya wachezaji kushindwa kuhimili ubora waliokuwa nao Ihefu hasa ukizingatia timu ya Young Africans imecheza takribani mechi 8 mfululizo pasipo kupumzika ndani ya mwezi mmoja.
Kocha Nabi alikipongeza pia kikosi cha Ihefu akisema kwamba kimejitahidi kutumia vyema udhaifu walikuwa nao Young Africans wakafanikiwa kupata matokeo. Aliongeza kuwa kupoteza mchezo huo kutawasaidia kuongeza umakini zaidi kwenye michezo iliyobaki na kwamba ni bora wamefungwa mapema ili wajipange sawa sawa kusahihisha makosa yao.
Kwa upande wa Juma Mwambusi, kocha wa Ihefu alisema kwamba alijua fika ubora wa Young Africans ni katikati, naye akaamua kuwapanga viungo wengi zaidi ili kuweza kuwavuruga na kutibua mipango yao jambo ambalo anashukuru wachezaji wake walilifanya kwa umakini mkubwa hatimaye kufanikisha kupata ushindi huo wa mabao mawili kwa moja ambao ni muhimu mno kwao.
Baada ya mchezo huo Ihefu inapanda nakushika nafasi ya 13 akiwa na alama 11 baada ya kucheza michezo 14 huku Young Africans wakiendelea kushika usikani na alama zao 32 wakiwa wameshuka uwanjani mara 13.