JKT Queens, Simba Queens Fainali Ngao ya Jamii

Michezo miwili ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii 2023 kwa wanawake Imemalizika kwa timu ya JKT Queens na Simba Queens kufuzu hatua ya fainali baada ya ushindi waliopata kwenye hatua ya nusu fainali.

Michezo hiyo miwili iliyopigwa Disemba 9, 2023 kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi ilimalizika kwa timu ya JKT Queens kupata ushindi wa magoli 5-0 dhidi ya Fountain Gate Princess kwenye nusu fainali ya kwanza na baadae Simba Queens akiifuata JKT baada ya kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati Simba Queens 5-4 Yanga Princess kwenye nusu fainali ya pili dhidi ya Yanga Princess.

Kocha mkuu JKT Queens Esther Chabruma alisema licha ya ushindi huo walioupata bado wachezaji wake wanafatiki kutokana na kuwa kwenye majukumu ya mechi nyingine hivi karibuni ndio sababu hawakucheza kwa ubora walioanza nao kipindi cha kwanza hata kutopata goli lolote kipindi cha pili.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa ushindi na kujituma licha ya fatiki waliyonayo, tumekuwa na muda mfupi wa kujiandaa kabla ya mchezo huu, hata hivyo pia niwapongeze wapinzani wangu wamekuwa bora kwenye kipindi cha pili”

Naye kocha wa msaidizi wa Simba Queens Musa Mgosi baada ya ushindi wa mikwaju ya penati na kujithibitishia kufuzu kucheza fainali alisema mchezo huo ulikuwa mgumu kutokana na ubora wa timu zote huku akiwapongeza wachezaji wake kwa kupata ushindi kwenye mchezo huo.

“Tumewaona JKT Queens kwenye mchezo wao hivyo Tutakwenda kuzitatua changamoto tulizoziona leo sambamba na kuwaongezea baadhi ya wachezaji ambao leo wamekosekana kutokana na kuchelewa kutoka kwenye majukumu ya timu zao za taifa, lakini nawahakikishia mashabiki wa Simba kwenda kuiona timu yao iliyobora zaidi na naamini tutafanya vizuri kwenye mchezo wa fainali” alisema Mgosi.

Michezo mingine ya Ngao ya Jamii inatarajiwa kupigwa Disemba 12, 2023 kwa mchezo wa fainali utakao zikutanisha Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Serengeti Lite JKT Queens na Simba Queens huku mchezo mwingine wa kumtafuta mshindi wa tatu ukizikutanisha timu ya Fountain Gate Princess na Yanga Princess.

Hata hivyo mechi mechi mbili za mwisho zitafuatiwa na sherehe za ubingwa ambapo bingwa ukiachilia mbali kubeba Kombe la mashindano hayo (Ngao ya jamii) pia atajibebea zawadi ya fedha taslimu shilingi 1000,000 zilizo tolewa na mdhamini wa michuano hiyo Vodacom Tanzania.