JKT Queens Yajinasibu Kutetea Ubingwa TWPL

Timu ya JKT Queens imetamba kutetea ubingwa wa ligi kuu ya wanawake kwa mara nyingine, ikiwa tu ni kufuatia ushindi walioupata kwenye mchezo wake wa raundi ya sita dhidi ya Yanga Princess Januari 22, 2024 uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Mchezo huo uliomalizika kwa ubao wa matokeo kumalizika ukisomeka Yanga Princess 1-3 JKT Queens matokeo ambayo yamemfanya kocha mkuu wa timu hiyo Esther Chabruma kusimama kifua mbele na kusema mwendelezo wa matokeo ya ushindi ndio yanaifanya timu yao kuzidi kujihakikishia kufikia nchi yao ya ahadi, ambayo ni kutetea ubingwa kwa kubeba ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya pili mfululizo.

Hata hivyo, licha ya JKT Queens kupata bao la kutangulia kwenye dakika za mapema na hata timu hizo kwenda mapumziko matokeo yakiwa Yanga Princess 0-2 JKT Queens. Matokeo hayo hayakuwavunja moyo wapinzani wao na badala yake Yanga Princess wakatumia muda wa mapumziko kwa kubadili baadhi ya mbinu.

Kipindi cha pili timu hizo zote zilitoshana nguvu kwa kufungana moja kila mmoja huku JKT Queens wakiwa ndiwaliofaidika zaidi na matokeo ya awali, kipyenga cha mwisho cha mwamuzi Tatu Malogo kilisikika wakati matokeo tlyakiwa ni Yanga Princess 1-3 JKT Queens.

Mbali na mchezo huo pia timu nyingine zote za ligi kuu ya wanawake zilikuwa zikimenyana katika madimba mbalimbali, wakati Simba Queens inayo shika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikivutwa shati ugenini dhidi ya Bunda Queens kwa suluhu ya 0-0, Allience Girls yenyewe kwenye uwanja wa nyumbani ilishindwa kuizui timu ya Baobab Queens wakapoteza kwa 1-2.

Matokeo mengine yakiwa ni; Ceasiaa Queens 2-0 Amani Queens, Geita Gold Queens 2-2 Fountain Gate Princess. Kwa matokeo hayo mpaka raundi hiyo JKT Queens inaongoza kileleni kwa alama 15 huku ikiwa na akiba ya mchezo mmoja, wakati Geita Gold Queens ikiwa ndio timu inayoburuza mkia kwa alama moja pekee.

Mechi nyingine za raundi ya saba zinatarajiwa kupigwa tarehe 26 na 27 mwezi huu Januari, 2024.