Kagera Mambo Safi, KMC Yabanwa Mbavu Nyumbani

Michezo miwili ya Ligi Kuu ya NBC ilipigwa Novemba 28, 2022 kwenye viwanja viwili tofauti Dar es Salaam na Mwanza ambapo timu ya Kagera Sugar ilifanikiwa kuiadhibu Mtibwa Sugar kwa bao 1-0 huku KMC wao wakishindwa kutamba kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Mchezo wa kwanza ulichezwa majira ya saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza ukizikutanisha Kagera na Mtibwa Sugar huku ule wa KMC dhidi ya Tanzania Prisons ukipigwa jijini Dar es Salaam katika dimba la Uhuru mnamo majira ya saa 10:00 jioni.

Kagera Sugar ilifanikiwa kupata bao lake la kuongoza dakika ya 69 kipindi cha pili, bao hilo likifungwa na Meshack Abraham. Bao hilo la Meshack ndiyo lililodumu mpaka dakika 90 za mchezo huo zinatamatika.

Kocha wa Kagera Sugar Mecky Mexime alisema timu yake ilicheza vyema kwa kujituma licha ya kushindwa kuzitumia nafasi kadhaa ilizozitengeneza. Aliongeza kuwa kikosi chake kilijiandaa kukabiliana na Mtibwa kwa tahadhali kubwa kwa kuwa yeye pamoja na benchi lake la ufundi walifahamu fika ubora wa wapinzani wao kwenye mchezo huo. Kwa hiyo, waliwaandaa wachezaji kisaikolojia kimbinu na kiutimamu wa mwili kwa lengo la kupata alama tatu katika mchezo huo ambao kwao ulikuwa na umuhimu mkubwa.

Kwa upande wa kocha wa Mtibwa Sugar Salum Mayanga alisema kikosi chake kilicheza vyema licha ya kupoteza mchezo huo akidai kuwa mpira ndivyo ulivyo kwani kila timu imejipanga kupata matokeo mazuri katika kila mchezo lakini kinachotokea uwanjani ni makosa yakimpira hivyo wao wataendelea kuimarisha palipo na udhaifu na kujipanga zaidi ili kufanikisha adhima yao.

Kwa upande wa makocho wa KMC na Tanzania Prisons nao walielezea tathimini ya mchezo baada ya kutoka suluhu tasa kwenye uwanja wa Uhuru. Shaban Mtupha kocha msaidizi wa Prisons alisema kupata alama moja kwao inafaida kubwa na itarudisha morali kwa wachezaji hivyo kuweza kufanya vizuri kwenye michezo inayofuata.

Naye Thiery Hitimana wa KMC alieleza kuwa kikosi chao kilijitahidi kutafuta matokeo ya ushindi lakini mfumo walioingia nao Prisons wa kujilinda zaidi ulikuwa ni kikwazo kwao. Hata hivyo, alidai kuwa kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza kumeathari mfumo wake. Pamoja na yote kocha Hitimana aliahidi kuendelea kupambana kukiandaa kikosi kwa kurekebisha baadhi ya makosa yaliyojitokeza kwenye michezo kadhaa iliyopita ambayo hakuweza kupata matokeo mazuri.