Kagera Sugar Yatangulia Fainali “NBC U20 PL”

Timu ya vijana U20 ya Kagera Sugar inayo shiriki fainali za Ligi kuu ya NBC kwa vijana chini ya miaka 20 imefanikiwa kuonyesha makali yake kwa kutangulia hatua ya fainali baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza, Fainali za Ligi kuu ya NBC U20 2023/2024.

Mchezo huo uliozikutanisha timu mwenyeji Simba SC na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi, Mei 22, 2024 majira ya saa 10:00 jioni ulimalizika kwa timu ya Kagera kubeba alama zote tatu muhimu za ushindi wa magoli 1-2.

Hata hivyo licha ya mchezo huo kuwa mgumu kwa pande zote mbili, bado matokeo yalikwenda kutafsiri mafanikio ya mbinu za kocha wa Kagera Sugar na kikosi chake kutokana na ushindi walioupata licha ya kuruhusu bao moja ambalo ndio bao pekee waliloruhusu kwenye fainali hizo.

Aidha kwenye mchezo huo pia magoli mawili ya Kagera Sugar yalifungwa na Khassim Feka, goli la kwanza likikwama kimyani kipindi cha kwanza kabla ya nyota huyo kurejea kumsalimia mlinda mlango wa Simba SC kwa mara nyingine ya pili. Huku goli pekee la Simba SC likifungwa na Isaya Ernest.

Akizungumza baada ya mchezo huo kocha Mkuu wa Simba SC Mohamed Mrishona aliwapongeza wapinzani Kwa kuonyesha ushindani dhidi yao, huku akisema bado wanayo nafasi ya kuipigania nafasi ya tatu Kwa msimu huu.

Kwa upande wa kocha Mkuu wa Kagera Sugar Raymond Dotto mwenyewe aliwapongeza vijana wake Kwa kuwa bora na kufikia malengo yao ya kucheza Fainali huku akijinasibu kuwa kabakiza kazi ndogo na kwamba Kuna kila dalili za timu yao kuubeba ubingwa huo.

Sasa Kagera Sugar anamsubiri kati ya Azam FC au Dodoma Jiji ambao wanataraji Kukipiga Mei 23, 2024 Azam Complex Chamazi kwenye mchezo wa nusu Fainali ya pili.