MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, Meddie Kagere, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Mei wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.

Kagere ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Bigirimana Blaise wa Alliance FC ya Mwanza na Tariq Kiakala wa Biashara United ya Mara alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa mwezi huo wa Mei, Simba ilicheza michezo nane na kushinda minne, sare tatu na kupoteza mija, ambapo Kagere alitoa mchango mkubwa kwa timu yake akifunga mabao sita na kuifanya Simba ipande kutoka nafasi ya pili hadi ya kwanza na kutwaa ubingwa.

Kwa upande wa Bigirimana yeye aliiongoza Alliance iliyocheza mechi tano ikishinda tatu, sare moja na kupoteza moja, ambapo alifunga mabao mawili na timu yake ilipaa kutoka nafasi ya 17 hadi ya 11 katika msimamo wa ligi. Kiakala yeye aliiwezesha Biashara kushinda mchezo mmoja, sare mbili na kupoteza moja na kuepuka balaa la kushuka daraja.

Pia Kamati ya Tuzo, imemchagua Kocha Mkuu wa KMC, Etienne Ndayiragije kuwa Kocha Bora wa Mwezi Mei akiwashinda Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems na Kocha Mkuu wa Alliance, Malale Hamsini.

Ndayiragije aliiongoza KMC katika michezo mitano iliyocheza ikishinda minne na sare moja ikivuna pointi 13 kati ya 15, ikipaa kutoka nafasi ya sita hadi ya nne, wakati Aussems aliiongoza Simba katika michezo nane, ikishinda minne, sare tatu na kupoteza moja ikivuna pointi 15 kati ya 24.

Kwa upande wa Malale Hamsini aliiongoza Alliance katika michezo mitano ikishinda mitatu, sare moja na kufungwa moja ikivuna pointi 10 kati ya 15 na kupanda kutoka nafasi ya 17 hadi ya 11 katika msimamo wa ligi.

Washindi watazawadiwa sh. 1,000,000 (milioni moja) kila mmoja, kikombe (trophy) kutoka wadhamini wa tuzo hizo za mwezi Biko Sports pamoja na kisimbusi kutoka Azam TV wenye haki za matangazo ya televisheni ya Ligi Kuu.