Kaimu Balozi Nagunwa: Tushinde tuliheshimishe Taifa

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Bi Judica Nagunwa amewataka wachezaji wa timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20 ‘Tanzanite Queens’ kupambana kufa kupona katika mchezo wa mkondo wa pili wa kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Nigeria  ili kuliletea Taifa la Tanzania heshima katika tasnia ya Michezo .

Hayo ameyasema alipotembelea mazoezi ya Tanzanite Queens yaliyofanyika katika uwanja wa Mashood Abiola, Nigeria.

Kaimu Balozi alisema, soka la wanawake linakua  kwa Kasi sana kwa miaka ya hivi karibuni na Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vyema katika Ukanda CECAFA na Afrika kwa ujumla hivyo timu hiyo ina kila sababu ya kuhakikisha inapambana kwa Hali zote kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Nigeria.

” Kama mliweza kufuzu kombe la Dunia kwa wanawake chini ya miaka 17 basi  nina imani mna uwezo wa kufuzu tena katika awamu hii kutokana na kwamba asilimia kubwa ya wachezaji waliokuwa Serengeti Girls ndio ambao wako katika kikosi hiki cha Tanzanite Queens. Hakikisheni mnalinda heshima ya Tanzania kwa kupata ushindi katika mchezo huu na michezo mingine ijayo”. Alisema Nagunwa.

Tanzanite Queens itashuka dimbani jumapili ya Novemba 12, 2023 katika mchezo wa mkondo wa pili wa kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Nigeria katika uwanja wa Mashood Abiola, Abuja- Nigeria.