Kamati ya Olimpiki Tanzania Imefunguwa Mafunzo kwa Wadau wa Michezo
Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) imefunguwa mafunzo ya juu ya usimamizi wa michezo kwa wadau mbalimbali wa michezo Tanzania yatakayo jumuisha washiriki 16.
Mafunzo hayo yanayotarajia kuanza rasmi mwishoni mwa mwezi huu yamefunguliwa rasmi Agosti 5, 2023 kwenye ukumbi uliopo hoteli ya Tiffany Diamond jijini Dar es Salaam huku mgeni rasmi akiwa ni Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania Gulam Rashid.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo Rais wa Olimpiki Gulam Rashid alisema kuwa hii ni mara ya pili kuendesha mafunzo hayo ambayo lengo lake kubwa ni kupandisha michezo katika viwango vya juu zaidi hasa katika upande wa elimu.
“Hii ni mara ya pili kuendesha mafunzo haya ambayo tutakuwa na walimu wa michezo, viongozi mbalimbali wa michezo lengo likiwa ni kuwapatia elimu ya kusimamia vizuri shughuli za michezo nchini kwetu” alisema Gulam Rashid.
Wakati wa ufunguzi huo pia Rais Gulam alimkabidhi Kitabu cha Mwalimu Bora wa Soka Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred huku akiamini kwamba TFF itakuwa ni njia sahihi ya kufanya elimu hiyo iwafikie wengi zaidi hasa kwenye mpira wa miguu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred akiwa ni miongoni mwa wakufunzi watakao endesha mafunzo hayo alisema kuwa wamekutana na washiriki kwenye ufunguzi ili kuwapatia maelekezo washiriki hao kuhusu namna mafunzo hayo yatakavyofanyika kwa kipindi chote mpaka kukamilika kwa moduli zote 6, sambamba na kuwafahamu wakufunzi wote.
Wakufunzi wengine ni; Henry Tandau, Sunday Kayuni, Danny Msangi na Ingridy Kimario, mafunzo hayo yanatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu Agosti 2023 yakiwa na jumla ya moduli 6 zitakazofanyika kwenye mikoa 6 tofauti hapa nchini.