Want create site? Find Free WordPress Themes and plugins.

MCHEZAJI wa timu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, Jafari Kibaya amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2019/20, huku Zuberi Katwila pia wa Mtibwa Sugar akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Kibaya na Katwila walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita na Kamati ya Tuzo za VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa mwezi huo wa Oktoba, Mtibwa Sugar ilicheza michezo minne, ikishinda mitatu na kupoteza moja, ambapo iliifunga Ndanda bao 1-0 ugenini mjini Mtwara, ikashinda nyumbani mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania na pia ilishinda nyumbani mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union na ilifungwa ugenini na Namungo bao 1-0.

Kibaya alikuwa na kiwango kizuri uwanjani kwa mwezi huo akichangia kwa asilimia kubwa mafanikio hayo ya Mtibwa, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili, ambapo aliwashinda Gerald Mathias wa Mwadui na Ditram Nchimbi wa Polisi Tanzania alioingia nao fainali. Mtibwa ilipanda katika msimamo kutoka nafasi ya 19 mwezi Septemba hadi ya 11 mwishoni mwa Oktoba.

Kama ilivyokuwa kwa Kibaya, Gerald naye alikuwa na kiwango kizuri ikiwa ni pamoja na kufunga katika michezo mitatu kati ya minne ya timu yake, ambapo alifunga bao moja katika ushindi wa Mwadui wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, pia alifunga bao pekee katika mchezo wa Mwadui na Simba, alifunga tena katika mchezo ambao Mwadui ililala mabao 2-1 kwa Coastal Union mjini Tanga. Mchezo mwingine Mwadui ilifungwa bao 1-0 na Polisi.

Kwa upande wa Nchimbi alionesha kiwango kizuri kwa timu yake, ambapo alifunga hat trick katika mchezo ambao timu hiyo ilitoka sare ya mabao 3-3 na Yanga. Polisi ilicheza michezo mitano kwa mwezi huo, ambapo licha ya sare ya Yanga, iliifunga Mwadui bao 1-0, ikaifunga Singida United mabao 2-1, ikafungwa na Mtibwa Sugar mabao 2-0 na ikafungwa na Lipuli mabao 2-1.

Kwa upande wa Katwila aliwashinda Mecky Maxime wa Kagera Sugar na Madenge Omary wa Biashara United, ambapo Katwila aliiongoza timu yake katika michezo minne, akishinda mitatu na kupoteza mmoja na kupanda kutoka nafasi ya 19 hadi ya 11 katika msimamo, wakati Madenge aliiongoza Biashara United katika michezo mitatu ikishinda miwili na sare moja, hivyo kupanda kutoka nafasi ya 20 hadi ya 15 katika msimamo.

Maxime aliiongoza Kagera Sugar katika michezo mitatu ikishinda miwili na sare mmoja na timu hiyo kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom inayoshirikisha timu 20.

Kwa kutwaa tuzo hiyo, Kibaya atazawadiwa sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka Vodacom, na kisimbusi kutoka Azam TV ambao ndiyo wenye haki ya matangazo ya televisheni ya Ligi Kuu ya Vodacom.

Did you find apk for android? You can find new Free Android Games and apps.