King Kibadeni Mputa na Sanday Manara Wapata Neema ya Mipira Kutoka TFF.
Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF hii leo (20Feb, 2020) katika ofisi zake zilizopo Karume Dar es Salaam limekabidhi mipira kwa kituo cha kukuzia vipaji cha “KIBADENI INTERNATIONAL SOCCER ACADEMY” chenye makao makuu yake huko Chanika Sogo Ally, Dar kinachomilikiwa na nguli wa mpira Abdallah King Kibadeni Mputa.
Akiongea kwa niaba ya TFF mkurugenzi wa ufundi Oscar Mirambo amesema kuwa nia kubwa ya kutoa mipira hiyo ni kuwaunga mkono na kushirikiana nao katika wakongwe hao waliosakata kabumbu kwa mafanikio zaidi, katika juhudi za kukuza vipaji na kuendeleza soka la Tanzania.
Mkurugenzi huyo amewapongeza akina Kibadani na Manara na kusema kuwa kwa sababu wao ni watu wa mpira na kwamba wamecheza mpira kwa mafanikio makubwa katika ngazi ya vilabu na Taifa pia, basi ingependeza sana kuona yale mambo mazuri waliyokuwa wakiyafanya katika zama zao yakafanyika pia kwa kizazi hiki na hata kwa vizazi vijavyo pia.
Aidha, Abdallah Kibadeni aliyeambatana na Sunday Manara wamepokea mipira hiyo na kulishukuru sana shirikisho la mpira nchini TFF lililo chini ya uongozi madhubuti wa Rais wa sasa, Wallace Karia na Mtendaji wake mkuu ndugu Wilfred Kidao kwa kuwa na malengo anuai na mipango mikakati iliyomakini yenye kuonesha lengo la kuendelea kujitoa kikamilifu katika kusaidia suala la kukuza vipaji na kuendeleza soka la vijana kwa ujumla.
Sunday Manara (Compyuta) aliongeza kwa kusema kuwa wao wakiwa wachezaji walio tumikia nchi kwa mda mrefu wanataka kuacha kumbukumbu katika soka kwa kuendeleza kituo hicho ili kiweze kuwa alama kubwa kwa vijana wengi wenye ndoto za kufika mbali katika medani hii ya mpira wa miguu;
Kwa kuwa mipira ndiyo vitendea kazi vya uwanjani, watatumia mipira hiyo kama nguzo katika kituo chao; kwa kuwa mipira ndio nyenzo mithili ya kalamu na daftari kwa mwanafunzi pindi awapo shuleni ama darasani.
Mbali na zawadi hiyo ya mipira, shirikisho la mpira Tanzania limewakabidhi pia hati za kusafiria nguli hao wawili ili kuwapa nafasi ya kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya maswala ya maendeleo ya soka nchini.
Kama kauli mbiu ya TFF isemavyo “Play Fair Be Positive”; yaani mpira ni mchezo wa kiungwana hivyo unapaswa kuchezwa kiungwana na watu wake hawana budi kuwa waungwana, ndivyo hivyo watani wa jadi hao wanaotoka katika vilabu viwili tofauti tena vilivyo na upenzani mkubwa nchini wanavyoonesha kuwa mpira sio vita wala uadui, bali ni burudani nafujo isiyoumiza.
Mfalme Mputa na Computa wameonesha kitendao cha ungwana kwa kuungana na kuanzisha kituo hicho cha kufundisha mpira huku wote wawili wakiwa tayari kabisa kutoa ujuzi walionao na kuwarithisha vijana wa Kitanzania kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.