Ushindi au sare dhidi ya Sudan kesho katika Uwanja wa KCCA, utaifanya timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kutinga kwa mara ya 15 katika hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Chalenji.
Mashindano hayo ambayo mwaka huu yanafanyika nchini Uganda, yanasimamiwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yakishirikisha nchi wanachama wake.
Kilimanjaro Stars ikiwa itaibuka na ushindi kesho dhidi ya Sudan katika mchezo utakaochezwa kuanzia saa 10 jioni, itafikisha pointi sita ambazo zitaifanya iungane na Kenya kwenda hatua ya nusu fainali kutokea kundi B.
Lakini matokeo ya sare pia yataivusha Kilimanjaro Stars hata ikiwa Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ itaibuka na ushindi dhidi ya Kenya kwani zote zitamaliza zikiwa na pointi nne lakini Kilimanjaro Stars itasonga mbele kwa faida ya kuwa na matokeo bora dhidi ya ndugu yake Zanzibar Heroes.
Ikiwa hilo litatimia, Kili Stars itakuwa inatinga nusu fainali ya mashindano hayo kwa mara ya 15 tangu muundo wake ulipobadilishwa mwaka 1973.
Hadi sasa Kilimanjaro Stars imeshanusa hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Chalenji mara 14 pindi yalipofanyika katika nyakati na nchi tofauti.
Mara ya kwanza kwa Stars kutinga hatua hiyo ilikuwa ni mwaka 1975 pindi yalipofanyika nchini Zambia, ambapo ilipenya na kutinga fainali ambako ilienda kupoteza mbele ya Kenya kwa mabao 3-2.
Baada ya hapo, Kilimanjaro Stars ilifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali katika miaka ya 1979, 1980, 1981, 1990, 1992, 1994, 2002, 2008, 2009, 2010, 2011, 2012 na 2013.
Kuthibitisha kuwa haikubahatisha kutinga hatua hiyo, ni mara tano tu ndio Stars ilifika nusu fainali pindi mashindano hayo yalipoandaliwa katika ardhi ya Tanzania Bara na mara tisa zilizobakia ilifanya hivyo ikiwa nje.
Nchini Kenya imefanya hivyo mara nne ambapo kati ya hizo, moja ikatwaa ubingwa napo ni mwaka 1994, imefanya hivyo nchini Uganda mara mbili, na mara mojamoja katika ardhi za Zambia, Sudan na Zanzibar.