KMC Mbeya City Zatoshana Nguvu Uhuru

Mchezo uliozikutanisha timu ya Manispaa ya Halmashauri ya Kinondoni (KMC) dhidi ya timu ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya (Mbeya City) ulimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1.

Mchezo huo wa kukamilisha duru ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa timu hizo ulipigwa Disemab1, 2022 kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam ambapo timu hizo licha ya kila timu kuhitaji matokeo kwa hali na mali ili kuweza kumaliza mchezo wa 15 kwa ushindi bado hakuna iliyoweza kuibuka na alama hizo tatu.

Katika mchezo huo KMC FC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza, bao lililofungwa na mchezaji Ibrahim Ame katika dakika ya 28. Kabla ya kwenda kwenye mapumziko, Mbeya City nao wakajibu mapigo kwa kupachika bao safi kupitia kwa Richardson Ng’ondya, aliyekwamisha kimiani bao hilo kunako dakika ya 35 kipindi cha kwanza na kuwafanya KMC kushindwa la kufanya mpaka kipyenga cha mwisho cha mwamuzi.

Akizungumza baada ya mchezo huo kocha wa KMC Tiery Hitimana alisema mchezo ulikuwa mgumu na kwamba wachezaji wake walifanya kila waliloliweza kwa nafasi yao wakapata goli la kuongoza. Bahati mbaya kupungua kwa umakini kulipelekea wao kufanya makosa yaliyosababisha Mbeya City kupata bao la kusawazisha, jambo ambalo limewaharibia mipango yao ya kutoka na alama tatu ambazo zilikuwa na umuhimu mkubwa kwao.

Naye kocha wa Mbeya City Mubiru Abdallah alisema kuwa anashukuru wachezaji wake kwa kujituma uwanjani na kuweza kupata bao la kusawazisha lililowapatia alama moja ambayo kwao inaumuhimu mkubwa kutokana na wao kuwa ugenini lakini pia kwa jinsi kila timu ilivyojipanga kuondoka na ushindi. Aliongeza na kusema kuwa ni ngumu kwenda uwanjani ukiwa na uhakika wa alama zote tatu kwa ligi ya sasa.

Kocha huyo alisema kuwa haridhishwi na kasumba ya baadhi ya wachezaji kuridhika mapema katika kusaka matokeo hasa baada ya kusawazisha bao tu; wengi huona kama wameumaliza mchezo jambo hilo kwake anaona haliko sawa hivyo ni lazima afanye kazi kubwa ya kuibadili hiyo tabia, kwa kuwa yeye na benchi la ufundi lote wanamipango mikubwa kwa timu hiyo.

Hata hivyo, alisema kuwa mchezo huo wa 15 wa ligi umekwisha na kwamba kilichobaki kwao ni kwenda kujipanga vyema zaidi kwa ajili ya duru ya ili kikosi hicho kiweze kushika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Msimu huu.

Ligi Kuu ya NBC Msimu wa 2022/2023 imezidi kuimarika zaidi baada ya kila timu kufanya usajili wa mzuri kulingana na mahitaji ya mabenchi yao ya ufundi kwa kuzingatia ushindani uliopo kwenye ligi ya Tanzania Bara. Hii inachagizwa pia na uwekezaji mkubwa uliofanya na Azam Media Ltd, TBC na Mdhamini Mkuu benki ya NBC.

Michezo mingine ya kuelekea kukamilisha duru ya kwanza itachezwa Disemba 2, 3 na 4 2022 huku michezo ya kukamilisha duru hiyo ikitarajiwa kuhitimishwa wiki ijayo.